Matendo ya machukizo
9 Mtakapoingia katika nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa, msijifunze kuiga njia za machukizo za mataifa ya huko. 10 Asionekane mtu yeyote miongoni mwenu ampitishaye mwanawe au binti yake katika moto, atakayefanya uaguzi, ulozi, anayetabiri nyakati, anayejishughulisha na uchawi, 11 wala arogaye kwa kupiga mafundo, wala mwaguzi au anayeabudu mizimu, wala awaombaye wafu. 12 Mtu yeyote afanyaye mambo haya ni chukizo kwa Mwenyezi Mungu, tena ni kwa sababu ya matendo haya ya kuchukiza wayafanyayo ndiyo maana Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atayafukuza mataifa hayo mbele yenu.