Shukrani na maombi
15 Kwa sababu hii, tangu niliposikia kuhusu imani yenu katika Bwana Isa na upendo wenu kwa watakatifu wote, 16 sijaacha kumshukuru Mungu kwa ajili yenu, nikiwakumbuka katika maombi yangu. 17 Nazidi kumwomba Mungu wa Bwana wetu Isa Al-Masihi, Baba wa utukufu, awajalieni ninyi roho ya hekima na ya ufunuo, ili mpate kumjua zaidi. 18 Ninaomba pia kwamba macho ya mioyo yenu yatiwe nuru ili mpate kujua tumaini mliloitiwa, utajiri wa urithi wa utukufu wake kwa watakatifu 19 na uweza wake mkuu usiolinganishwa kwa ajili yetu sisi tuaminio. Uweza huo unaofanya kazi ndani yetu, ni sawa na ile nguvu kuu mno 20 aliyoitumia katika Al-Masihi alipomfufua kutoka kwa wafu, na kumketisha mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho, 21 juu sana kuliko falme zote na mamlaka, enzi na milki, na juu ya kila jina litajwalo, si katika ulimwengu huu tu, bali katika ule ujao pia. 22 Naye Mungu ameweka vitu vyote viwe chini ya miguu yake, na amemfanya yeye awe kichwa cha vitu vyote kwa ajili ya jumuiya ya waumini, 23 ambayo ni mwili wake, ukamilifu wake yeye aliye yote katika yote.