11 Lakini Musa akamsihi Mwenyezi Mungu, Mungu wake, akasema, "Ee Mwenyezi Mungu, kwa nini hasira yako iwake dhidi ya watu wako, wale uliowatoa Misri kwa uweza mkuu na mkono wenye nguvu? 12 Kwa nini Wamisri waseme, ‘Ni kwa nia mbaya aliwatoa Misri, ili awaue milimani na kuwafuta usoni mwa dunia’? Achilia mbali hasira yako kali, waonee huruma na usilete maafa juu ya watu wako. 13 Wakumbuke watumishi wako Ibrahimu, Isaka na Israeli, ambao uliwaapia kwa nafsi yako mwenyewe: ‘Nitawafanya uzao wako kuwa wengi kama nyota za angani, nami nitawapa wazao wako nchi hii yote niliyowaahidia, nayo itakuwa urithi wao milele.’ " 14 Kisha Mwenyezi Mungu akawaonea huruma, wala hakuleta juu ya watu wake maafa aliyokuwa amekusudia.