Ng’aeni kama mianga katika ulimwengu
12 Kwa hiyo, wapendwa wangu, kama vile mmekuwa mkitii siku zote, si tu wakati nikiwa pamoja nanyi, bali sasa zaidi sana nisipokuwepo, utimizeni wokovu wenu kwa kuogopa na kutetemeka, 13 kwa maana Mungu ndiye atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu kwa kulitimiza kusudi lake jema.
14 Fanyeni mambo yote bila kunung’unika wala kushindana, 15 ili msiwe na lawama wala hatia, bali mwe wana wa Mungu wasio na kasoro katika kizazi chenye ukaidi na kilichopotoka, ambacho ndani yake ninyi mnang’aa kama mianga ulimwenguni. 16 Mkilishika neno la uzima, ili nipate kuona fahari siku ya Al-Masihi kwamba sikupiga mbio wala kujitaabisha bure.