Chukulianeni mizigo
1 Ndugu zangu, ikiwa mtu amepatikana akitenda dhambi, basi ninyi mnaoishi kwa Roho wa Mungu mnapaswa kumrejesha mtu huyo kwa upole. Lakini jihadharini, ili ninyi wenyewe msije mkajaribiwa. 2 Chukulianeni mizigo ninyi kwa ninyi, nanyi kwa njia hii mtatimiza sheria ya Al-Masihi. 3 Mtu yeyote akijiona kuwa yeye ni bora na kumbe sivyo, basi mtu huyo anajidanganya mwenyewe. 4 Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo aweze kujisifu, bila kujilinganisha na mtu mwingine. 5 Kwa maana, kila mtu atauchukua mzigo wake mwenyewe.