20 Mungu akasema, "Kuwepo na viumbe hai tele kwenye maji, nao ndege waruke juu ya dunia katika nafasi ya anga." 21 Kwa hiyo Mungu akaumba wanyama wakubwa wa baharini na kila kiumbe hai kiendacho majini kulingana na aina zake, na kila ndege mwenye mabawa kulingana na aina yake. Mungu akaona kuwa hili ni jema. 22 Mungu akavibariki, akasema, "Zaeni mwongezeke, mkayajaze maji ya bahari, nao ndege waongezeke katika dunia." 23 Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya tano.
24 Mungu akasema, "Ardhi na itoe viumbe hai kulingana na aina zake: mifugo, viumbe vinavyotambaa ardhini na wanyama pori, kila kiumbe kulingana na aina yake." Ikawa hivyo.