23 Ibrahimu akamsogelea, akasema: "Je, utawaangamiza wenye haki na waovu? 24 Je, ikiwa watakuwepo watu hamsini wenye haki katika mji huo, kweli utauangamiza na wala hutauacha kwa ajili ya hao watu hamsini wenye haki waliomo? 25 Na liwe mbali nawe, kufanya jambo kama hilo: kuwaua wenye haki pamoja na waovu, kuwatendea wenye haki sawasawa na waovu. Liwe mbali nawe! Je, Mwamuzi wa dunia yote hatafanya haki?"
26 Mwenyezi Mungu akajibu, "Nikipata watu hamsini wenye haki katika mji wa Sodoma, nitauacha huo mji wote kwa ajili yao."
27 Kisha Ibrahimu akasema tena: "Sasa kwa kuwa nimekuwa na ujasiri wa kuzungumza na Bwana, ingawa mimi si kitu bali ni mavumbi na majivu. 28 Je, kama hesabu ya wenye haki imepungua watano katika hamsini, utauangamiza huo mji wote kwa ajili ya hao watano waliopungua?"
Bwana akamjibu, "Nikiwakuta huko watu arobaini na watano, sitauangamiza."
29 Ibrahimu akazungumza naye kwa mara nyingine, "Je, kama huko watapatikana watu arobaini tu?"
Akamjibu, "Kwa ajili ya hao arobaini, sitauangamiza."
30 Ndipo akasema, "Bwana na asikasirike, lakini niruhusu nizungumze. Je, kama huko watakuwepo thelathini tu?"
Akajibu, "Sitauangamiza ikiwa nitawakuta huko watu thelathini."
31 Ibrahimu akasema, "Sasa kwa kuwa nimekuwa na ujasiri sana kuzungumza na Bwana, je, wakipatikana huko watu ishirini tu?"
Bwana akajibu, "Kwa ajili ya hao ishirini, sitauangamiza."
32 Ibrahimu akasema, "Bwana na asikasirike, lakini niruhusu nizungumze tena mara moja tu. Itakuwaje kama watapatikana huko watu kumi tu?"
Bwana akajibu, "Kwa ajili ya hao kumi, sitauangamiza."
33 Mwenyezi Mungu alipomaliza kuzungumza na Ibrahimu, akaondoka, naye Ibrahimu akarudi nyumbani.