Gharika kuu
1 Idadi ya watu ilipoanza kuongezeka duniani, na watoto wa kike wakazaliwa kwao, 2 wana wa Mungu wakawaona kuwa hao binti za wanadamu walikuwa wazuri wa sura, wakaoa yeyote miongoni mwao waliyemchagua. 3 Ndipo Mwenyezi Mungu akasema, "Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye ni wa kufa; siku zake zitakuwa miaka mia moja na ishirini."
4 Wanefili walikuwa duniani siku hizo, na hata baadaye, hao wana wa Mungu walipoingia kwa binti za wanadamu na kuzaa nao. Wanefili walikuwa mashujaa wa zamani, na watu mashuhuri.
5 Mwenyezi Mungu akaona jinsi uovu wa mwanadamu ulivyokuwa mkubwa duniani, na ya kuwa kila mwelekeo wa mawazo ya moyo wake wakati wote ulikuwa mbaya tu. 6 Mwenyezi Mungu akasikitika kwamba alimuumba mwanadamu duniani, na moyo wa Mungu ukasikitika sana. 7 Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akasema, "Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemuumba kutoka uso wa dunia, wanadamu na wanyama, pamoja na viumbe vinavyotambaa ardhini, na ndege wa angani. Kwa maana nasikitika kuwaumba." 8 Lakini Nuhu akapata kibali machoni pa Mwenyezi Mungu.
9 Hivi ndivyo vizazi vya Nuhu.
Nuhu alikuwa mtu wa haki, na mkamilifu miongoni mwa watu wa wakati wake, tena alitembea na Mungu.