6 Baada ya siku arobaini, Nuhu akafungua dirisha alilokuwa amelifanya katika safina, 7 akamtoa kunguru, naye akawa akiruka kwenda na kurudi hadi maji yalipokwisha kukauka juu ya dunia. 8 Kisha akamtoa hua ili aone kama maji yameondoka juu ya ardhi. 9 Lakini hua hakupata mahali pa kutua, kwa kuwa maji yalienea juu ya uso wa dunia yote, kwa hiyo akarudi kwa Nuhu ndani ya safina. Nuhu akanyoosha mkono akamchukua yule hua, akamrudisha ndani ya safina. 10 Nuhu akangojea siku saba zaidi, kisha akamtoa tena hua kutoka safina. 11 Jioni hua aliporudi kwa Nuhu alikuwa amebeba jani bichi la mzeituni lililochumwa wakati ule ule katika mdomo wake! Ndipo Nuhu akajua ya kuwa maji yameondoka juu ya dunia. 12 Akangojea siku saba zaidi na akamtuma tena hua, lakini wakati huu hua hakurudi tena kwa Nuhu.
Publicidade