16 Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine akae nanyi milele. 17 Huyo ndiye Roho wa kweli ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa sababu haumwoni wala haumjui. Ninyi mnamjua kwa kuwa yuko pamoja nanyi, naye anakaa ndani yenu. 18 Sitawaacha ninyi yatima; nitakuja kwenu. 19 Bado kitambo kidogo na ulimwengu hautaniona tena, ila ninyi mtaniona. Kwa kuwa mimi ni hai, ninyi nanyi mtakuwa hai. 20 Wakati huo mtajua ya kuwa mimi niko ndani ya Baba, na ninyi mko ndani yangu, na mimi niko ndani yenu. 21 Yeyote mwenye amri zangu na kuzishika ndiye anipendaye. Naye anipendaye atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake."
22 Ndipo Yuda (siyo Iskariote) akamwambia, "Bwana, itakuwaje kwamba utajidhihirisha kwetu na si kwa ulimwengu?"
23 Isa akamjibu, "Mtu yeyote akinipenda atalishika neno langu na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake na kufanya makao yetu kwake. 24 Mtu yeyote asiyenipenda hayashiki maneno yangu, na maneno niliyowapa si yangu bali ni ya Baba aliyenituma.
25 "Nimewaambia mambo haya yote wakati bado niko pamoja nanyi. 26 Lakini huyo Msaidizi, yaani huyo Roho Mtakatifu wa Mungu, ambaye Baba atamtuma kwenu kwa Jina langu, atawafundisha mambo yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia.