23 Askari walipokwisha kumsulubisha Isa, walichukua nguo zake wakazigawa mafungu manne, kila askari fungu lake. Ila walikubaliana wasilichane lile vazi lake kwa maana lilikuwa halina mshono, bali limefumwa tangu juu hadi chini.
24 Wakaambiana, "Tusilichane ila tulipigie kura ili kuamua ni nani atalichukua."
Hili lilitukia ili Maandiko yapate kutimizwa yale yaliyosema,
"Wanagawana nguo zangu,
na vazi langu wanalipigia kura."
Hayo ndiyo waliyoyafanya wale askari.
25 Karibu na msalaba wa Isa walikuwa wamesimama mama yake, na dada wa mamaye, na Mariamu mke wa Klopa, na Mariamu Magdalene. 26 Isa alipomwona mama yake mahali pale, na yule mwanafunzi aliyempenda akiwa amesimama karibu, Isa akamwambia mama yake, "Mama, huyu hapa ndiye mwanao." 27 Kisha akamwambia yule mwanafunzi, "Nawe huyu hapa ndiye mama yako." Tangu wakati huo yule mwanafunzi akamchukua mama yake Isa nyumbani mwake.