Isa amtokea Mariamu Magdalene
11 Lakini Mariamu Magdalene akasimama nje ya kaburi akilia. Alipokuwa akilia, akainama kuchungulia mle kaburini, 12 naye akaona malaika wawili wamevaa mavazi meupe, wameketi pale mwili wa Isa ulipokuwa umelazwa, mmoja upande wa kichwani na mwingine upande wa miguuni.
13 Wakamuuliza Mariamu, "Mwanamke, mbona unalia?"
Akawaambia, "Nalia kwa kuwa wamemchukua Bwana wangu, na sijui walikomweka." 14 Baada ya kusema hayo, akageuka, akamwona Isa amesimama, lakini hakumtambua.
15 Isa akamwambia, "Mwanamke, mbona unalia? Unamtafuta nani?"
Mariamu, akidhani alikuwa anaongea na mtunza bustani, akamwambia, "Bwana, kama ni wewe umemchukua, tafadhali nioneshe ulikomweka, nami nitamchukua."
16 Isa akamwita, "Mariamu!"
Ndipo Mariamu akamgeukia Isa na kusema naye kwa Kiebrania, "Raboni!" (maana yake "Mwalimu").
17 Isa akamwambia, "Usinishike, kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba20:17 Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yohana 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili.. Lakini nenda kwa ndugu zangu ukawaambie, ‘Ninapaa kwenda kwa Baba yangu ambaye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu ambaye ni Mungu wenu.’ "
18 Kwa hiyo Mariamu Magdalene akaenda kuwatangazia wanafunzi wa Isa, akisema, "Nimemwona Bwana!" Naye akawaambia kwamba Isa alikuwa amemweleza mambo hayo yote.