46 Hivyo Isa akafika tena Kana ya Galilaya, kule alikuwa amebadili maji kuwa divai. Kulikuwa na afisa mmoja wa mfalme, ambaye mwanawe alikuwa mgonjwa huko Kapernaumu. 47 Huyo mtu aliposikia kwamba Isa alikuwa amewasili Galilaya kutoka Yudea, alimwendea na kumsihi aende akamponye mwanawe, aliyekuwa mgonjwa karibu ya kufa.
48 Isa akamwambia, "Ninyi watu msipoona ishara na miujiza kamwe hamtaamini."
49 Yule afisa wa mfalme akamwambia, "Bwana, tafadhali shuka kabla mwanangu hajafa."
50 Isa akamjibu, "Nenda zako, mwanao yu hai."
Yule afisa akaamini yale maneno Isa aliyomwambia, akaenda zake. 51 Alipokuwa bado yuko njiani, akakutana na watumishi wake, wakamwambia kwamba mwanawe yu mzima. 52 Akawauliza saa ambayo alianza kupata nafuu. Wakamwambia, "Jana saa saba, ndipo homa iliisha."
53 Ndipo baba wa huyo mtoto akakumbuka kuwa huo ndio wakati Isa alikuwa amemwambia, "Mwanao yu hai." Kwa hiyo yeye na wote wa nyumbani mwake wakamwamini Isa.
54 Hii ilikuwa ishara ya pili ambayo Isa alifanya aliporudi Galilaya kutoka Yudea.