1 Basi malango ya Yeriko yalifungwa kwa uthabiti kwa sababu ya Waisraeli. Hakuna mtu yeyote aliyetoka au kuingia.
2 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Yoshua, "Tazama, nimeitia Yeriko mikononi mwako, pamoja na mfalme wake na wapiganaji wake. 3 Zunguka mji mara moja pamoja na watu wote wenye silaha. Fanya hivi kwa siku sita. 4 Uwe na makuhani saba wakibeba mabaragumu ya pembe za kondoo dume mbele ya Sanduku. Siku ya saba, mzunguke mji mara saba, nao makuhani wakipiga baragumu hizo. 5 Utakapowasikia wamepaliza sauti kubwa ya baragumu, watu wote wapige kelele kwa sauti kuu, kisha ukuta wa mji utaanguka na wapiganaji watapanda, kila mtu akielekea mbele yake."
6 Ndipo Yoshua mwana wa Nuni akaita makuhani na kuwaambia, "Chukueni Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu na makuhani saba wachukue baragumu za pembe za kondoo dume mbele yake." 7 Naye akawaagiza watu, "Songeni mbele! Mkauzunguke mji, na walinzi wenye silaha watangulie mbele ya Sanduku la Mwenyezi Mungu."