Unabii wa Zakaria
67 Zakaria, baba yake, akajazwa na Roho Mtakatifu wa Mungu, naye akatoa unabii, akisema:
68 "Ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli,
kwa kuwa amewajilia watu wake na kuwakomboa.
69 Naye ametusimamishia pembe1:69 pembe inamaanisha nguvu ya wokovu
katika nyumba ya Daudi mtumishi wake,
70 (kama alivyonena kwa vinywa vya manabii wake
watakatifu tangu zamani),
71 kwamba atatuokoa kutoka kwa adui zetu,
na kutoka mikononi mwao wote watuchukiao:
72 ili kuonesha rehema kwa baba zetu
na kukumbuka agano lake takatifu,
73 kiapo alichomwapia baba yetu Ibrahimu:
74 kutuokoa kutoka mikononi mwa adui zetu,
tupate kumtumikia yeye pasipo hofu
75 katika utakatifu na haki mbele zake,
siku zetu zote.
76 "Nawe mtoto wangu, utaitwa nabii wa Aliye Juu Sana;
kwa kuwa utamtangulia Mwenyezi Mungu
na kuandaa njia kwa ajili yake,
77 kuwajulisha watu wake wokovu
utakaopatikana kwa kusamehewa dhambi zao,
78 kwa ajili ya wingi wa rehema za Mungu wetu,
nuru inayotoka juu itatuzukia
79 ili kuwaangazia wale wanaoishi gizani
na katika uvuli wa mauti,
kuiongoza miguu yetu katika njia ya amani."