Mfano wa Msamaria mwema
25 Wakati huo mtaalamu mmoja wa Torati alisimama ili kumjaribu Isa, akamuuliza, "Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?"
26 Isa akamjibu, "Imeandikwaje katika Torati? Kwani unasoma nini humo?"
27 Akajibu, " ‘Mpende Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote’; tena, ‘Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.’ "
28 Isa akamwambia, "Umejibu vyema. Fanya hivyo nawe utaishi."
29 Lakini yule mtaalamu wa Torati, akitaka kujionesha kuwa mwenye haki, akamuuliza Isa, "Jirani yangu ni nani?"
30 Isa akamjibu akasema, "Mtu mmoja alikuwa akiteremka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko, naye akaangukia mikononi mwa wanyang’anyi. Wakampiga, wakaondoka, wakamwacha akiwa karibu kufa. 31 Kuhani mmoja alikuwa akipitia njia ile, alipomwona huyo mtu, akapita upande mwingine, akamwacha hapo barabarani. 32 Vivyo hivyo, Mlawi mmoja naye alipofika mahali pale, alimwona, akapita upande mwingine, akamwacha hapo barabarani. 33 Lakini Msamaria mmoja aliyekuwa akisafiri alipomwona, alimhurumia. 34 Akaenda alipokuwa na akasafisha majeraha yake kwa divai na mafuta, kisha akayafunga. Ndipo akampandisha kwenye punda wake, akampeleka hadi kwenye nyumba ya wageni na kumtunza. 35 Kesho yake, yule Msamaria akachukua dinari mbili10:35 Dinari mbili ni sawa na mshahara wa kibarua wa siku mbili. akampa yule mwenye nyumba ya wageni na kusema, ‘Mtunze, nami nirudipo nitakulipa gharama yoyote ya ziada uliyotumia kwa ajili yake.’
36 "Ni yupi basi miongoni mwa hawa watatu wewe unadhani ni jirani yake yule mtu aliyeangukia mikononi mwa wanyang’anyi?"
37 Yule mtaalamu wa Torati akajibu, "Ni yule aliyemhurumia."
Ndipo Isa akamwambia, "Nenda, ukafanye vivyo hivyo."