16 Kisha akawaambia mfano huu: "Shamba la mtu mmoja tajiri lilizaa sana. 17 Akawaza moyoni mwake, ‘Nifanye nini? Sina mahali pa kuhifadhi mavuno yangu.’
18 "Ndipo huyo tajiri akasema, ‘Nitafanya hivi: Nitabomoa maghala yangu ya nafaka na kujenga mengine makubwa zaidi na nihifadhi mavuno yangu yote na vitu vyangu. 19 Nami nitaiambia nafsi yangu, "Nafsi, unavyo vitu vingi vizuri ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi. Pumzika; kula, unywe, ufurahi." ’
20 "Lakini Mungu akamwambia, ‘Mpumbavu wewe! Usiku huu uhai wako unatakiwa. Sasa hivyo vitu ulivyojiwekea akiba vitakuwa vya nani?’
21 "Hivyo ndivyo ilivyo kwa wale wanaojiwekea mali lakini hawajitajirishi kwa Mungu."
Msiwe na wasiwasi
(Mathayo 6:25-34)