10 Basi Isa alikuwa akifundisha katika sinagogi13:10 Nyumba ya ibada na mafunzo. mojawapo siku ya Sabato. 11 Wakati huo huo akaja mwanamke mmoja aliyekuwa na pepo mchafu, naye alikuwa amepinda mgongo kwa muda wa miaka kumi na nane, wala alikuwa hawezi kunyooka wima. 12 Isa alipomwona, akamwita, akamwambia, "Mwanamke, uwe huru, umepona ugonjwa wako." 13 Isa alipomwekea mikono yake, akasimama wima mara moja, akaanza kumtukuza Mungu.
14 Lakini kiongozi wa sinagogi akakasirika kwa sababu Isa alikuwa ameponya mtu siku ya Sabato. Akaambia umati ule wa watu, "Kuna siku sita ambazo watu wanapaswa kufanya kazi. Katika siku hizo, njooni mponywe, lakini si katika siku ya Sabato."
15 Lakini Bwana Isa akamjibu, "Enyi wanafiki! Je, kila mmoja wenu hamfungulii ng’ombe wake au punda wake kutoka zizini akampeleka kumnywesha maji siku ya Sabato? 16 Je, huyu mwanamke, ambaye ni binti ya Ibrahimu, aliyeteswa na Shetani akiwa amemfunga kwa miaka yote hii kumi na nane, hakustahili kufunguliwa kutoka kifungo hicho siku ya Sabato?"
17 Aliposema haya, wapinzani wake wakaaibika, lakini watu wakafurahi kwa ajili ya mambo ya ajabu aliyoyafanya.