Isa amponya kipofu karibu na Yeriko
35 Isa alipokuwa anakaribia Yeriko, kipofu mmoja alikuwa ameketi kando ya njia akiomba msaada. 36 Kipofu huyo aliposikia umati wa watu wakipita, akauliza nini kilikuwa kikitendeka. 37 Wakamwambia, "Isa Al-Nasiri anapita."
38 Akapaza sauti, akasema, "Isa, Mwana wa Daudi18:38 Ina maana kwamba Isa ni mrithi wa kiti cha enzi cha Mwenyezi Mungu (Zaburi 89:3-4)., nihurumie!"
39 Wale waliokuwa wametangulia mbele wakamkemea, wakamwambia akae kimya. Lakini yeye akapaza sauti zaidi, "Mwana wa Daudi, nihurumie!"
40 Isa akasimama, akawaamuru wamlete huyo mtu kwake. Alipokaribia, Isa akamuuliza, 41 "Unataka nikufanyie nini?"
Akajibu, "Bwana, nataka kuona."
42 Isa akamwambia, "Basi upate kuona. Imani yako imekuponya." 43 Akapata kuona mara hiyo, akamfuata Isa, huku akimsifu Mungu. Watu wote walipoona mambo hayo, nao wakamsifu Mungu.