Pular para o conteúdo
Publicidade

Luka 2

Isa apelekwa Hekaluni

22 Ulipotimia wakati wa utakaso wake Mariamu kwa mujibu wa Torati ya Musa, basi Yusufu na Mariamu walimpeleka mtoto Yerusalemu, ili kumweka wakfu kwa Mwenyezi Mungu 23 (kama ilivyoandikwa katika Torati ya Mwenyezi Mungu, kwamba, "Kila mtoto wa kiume kifungua mimba atawekwa wakfu kwa Mwenyezi Mungu"), 24 na pia kutoa dhabihu kulingana na yale yaliyonenwa katika Torati ya Mwenyezi Mungu: "Hua wawili au makinda wawili wa njiwa".

25 Basi huko Yerusalemu kulikuwa mtu mmoja aliyeitwa Simeoni, aliyekuwa mwenye haki na mcha Mungu. Alikuwa akitazamia faraja ya Israeli, na Roho Mtakatifu wa Mungu alikuwa juu yake. 26 Roho wa Mungu alikuwa amemfunulia kuwa hatakufa kabla hajamwona Al-Masihi wa Bwana. 27 Simeoni, akiwa ameongozwa na Roho wa Mungu, alienda Hekaluni. Wazazi walipomleta mtoto Isa ili kumfanyia kama ilivyokuwa desturi ya Torati, 28 ndipo Simeoni akampokea mtoto mikononi mwake na kumsifu Mungu, akisema:

29 "Bwana Mungu Mwenyezi, kama ulivyoahidi,

sasa mruhusu mtumishi wako

aende kwa amani.

30 Kwa maana macho yangu yameuona wokovu wako,

31 ulioweka tayari machoni pa watu wote,

32 nuru kwa ajili ya ufunuo kwa watu wa Mataifa

na kwa ajili ya utukufu kwa watu wako Israeli."

33 Naye Yusufu na mama yake mtoto wakastaajabu kwa yale yaliyokuwa yamesemwa kumhusu huyo mtoto. 34 Kisha Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, "Mtoto huyu amewekwa kwa makusudi ya kuanguka na kuinuka kwa wengi katika Israeli. Atakuwa ishara ambayo watu watanena dhidi yake, 35 ili mawazo ya mioyo mingi yadhihirike. Nao upanga utauchoma moyo wako."

36 Tena alikuwako Hekaluni nabii mmoja mwanamke, jina lake Ana binti Fanueli, wa kabila la Asheri. Alikuwa mzee sana; naye alikuwa ameolewa na kuishi na mume kwa miaka saba tu, kisha mumewe akafa. 37 Hivyo alikuwa mjane na umri wake ulikuwa miaka themanini na nne. Yeye hakuondoka humo Hekaluni usiku wala mchana, bali alikuwa akimwabudu Mungu, akifunga na kuomba. 38 Wakati huo huo, Ana alikuja akaanza kusifu, akimshukuru Mungu na kusema habari za huyo mtoto kwa watu wote waliokuwa wakitarajia ukombozi wa Yerusalemu.

Veja também