Isa awatokea wanafunzi wawili
13 Ikawa siku hiyo hiyo, wanafunzi wawili wa Isa walikuwa njiani wakienda kijiji kilichoitwa Emau, yapata maili saba24:13 kama kilomita 11 kutoka Yerusalemu. 14 Walikuwa wakizungumza wao kwa wao kuhusu mambo yote yaliyotukia. 15 Walipokuwa wakizungumza na kujadiliana, Isa mwenyewe akaja akatembea pamoja nao, 16 lakini macho yao yakazuiliwa ili wasimtambue.
17 Akawauliza, "Ni mambo gani haya mnayozungumza wakati mnatembea?"
Wakasimama, nyuso zao zikionesha huzuni. 18 Mmoja wao, aliyeitwa Kleopa, akamuuliza, "Je, wewe ndiwe peke yako mgeni huku Yerusalemu, ambaye hufahamu mambo yaliyotukia humo siku hizi?"
19 Akawauliza, "Mambo gani?"
Wakamjibu, "Mambo ya Isa Al-Nasiri. Yeye alikuwa nabii, mwenye uwezo mkuu katika maneno yake na matendo yake, mbele za Mungu na mbele ya wanadamu wote. 20 Viongozi wa makuhani na viongozi wetu walimtoa ahukumiwe kufa, nao wakamsulubisha. 21 Lakini tulikuwa tumetegemea kwamba yeye ndiye atakayewakomboa Israeli. Zaidi ya hayo, leo ni siku ya tatu tangu mambo haya yatendeke. 22 Isitoshe, baadhi ya wanawake katika kundi letu wametushtusha. Walienda kaburini leo alfajiri, 23 lakini hawakuukuta mwili wake. Walirudi wakasema wameona maono ya malaika ambao waliwaambia kwamba Isa yu hai. 24 Kisha baadhi ya wenzetu walienda kaburini wakalikuta kama vile wale wanawake walivyokuwa wamesema, lakini yeye hawakumwona."
25 Isa akawaambia, "Ninyi ni wajinga kiasi gani, nanyi ni wazito mioyoni mwenu kuamini mambo yote yaliyonenwa na manabii! 26 Je, haikumpasa Al-Masihi24:26 Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta. kuteswa kwa njia hiyo na kisha aingie katika utukufu wake?" 27 Naye akianzia na Torati ya Musa na Manabii wote, akawafafanulia jinsi Maandiko yalivyosema kumhusu.
28 Nao walipokaribia kile kijiji walichokuwa wakienda, Isa akawa kama anaendelea mbele. 29 Lakini wao wakamsihi sana akae nao, wakisema, "Kaa hapa nasi, kwa maana sasa ni jioni na usiku unaingia." Basi akaingia ndani kukaa nao.
30 Alipokuwa mezani pamoja nao, akachukua mkate, akashukuru, akaumega, akaanza kuwagawia. 31 Ndipo macho yao yakafumbuliwa, nao wakamtambua, naye akatoweka machoni pao. Hawakumwona tena. 32 Wakaulizana wao kwa wao, "Je, mioyo yetu haikuwaka ndani yetu alipokuwa anazungumza nasi njiani na kutufafanulia Maandiko?"
33 Wakaondoka mara hiyo, wakarudi Yerusalemu. Wakawakuta wale wanafunzi kumi na mmoja na wale waliokuwa pamoja nao wamekusanyika, 34 wakasema, "Ni kweli! Bwana Isa amefufuka, naye amemtokea Simoni." 35 Kisha wale wanafunzi wawili wakaeleza yaliyotukia njiani na jinsi walivyomtambua Isa alipoumega mkate.