31 Isa akawauliza, "Niwafananishe na nini watu wa kizazi hiki? Wanafanana na nini? 32 Wao ni kama watoto waliokaa sokoni wakiitana wao kwa wao, wakisema:
" ‘Tuliwapigia filimbi,
lakini hamkucheza;
tuliwaimbia nyimbo za maombolezo,
lakini hamkulia.’
33 Kwa maana Yahya alikuja, alikuwa hali mkate wala hanywi divai, nanyi mkasema, ‘Yeye ana pepo mchafu.’ 34 Mwana wa Adamu alikuja akila na kunywa, nanyi mnasema: ‘Tazameni huyu mlafi na mlevi, rafiki wa watoza ushuru na "wenye dhambi." ’ 35 Lakini hekima huthibitishwa kuwa kweli na watoto wake wote."
Isa apakwa mafuta na mwanamke mwenye dhambi
36 Basi Farisayo mmoja alimwalika Isa kwake ale chakula. Hivyo Isa akaenda nyumbani mwa yule Farisayo na kuketi mezani. 37 Palikuwa na mwanamke mmoja katika mji ule aliyekuwa mwenye dhambi. Alipopata habari kwamba Isa alikuwa akila chakula nyumbani mwa yule Farisayo, akaleta chupa ya marhamu yenye manukato.