Pular para o conteúdo
Publicidade

Lucas 9

Isa alisha wanaume 5,000

10 Mitume wake waliporudi, wakamweleza Isa yote waliyofanya. Kisha akaenda nao faraghani hadi mji uitwao Bethsaida. 11 Lakini umati wa watu wakafahamu alikoenda, wakamfuata. Akawakaribisha na kunena nao kuhusu ufalme wa Mungu na kuwaponya wale wote waliokuwa wanahitaji uponyaji.

12 Ilipokaribia jioni, wale mitume kumi na wawili wakaenda kwa Isa na kumwambia, "Waage watu hawa ili waende vijijini jirani na mashambani, ili wapate chakula na mahali pa kulala, kwa maana hapa tuko nyikani."

13 Isa akawajibu, "Ninyi wapeni chakula."

Nao wakajibu, "Tuna mikate mitano na samaki wawili tu. Labda twende tukanunue chakula cha kuwatosha watu hawa wote." 14 (Walikuwepo wanaume wapatao elfu tano.)

Isa akawaambia wanafunzi wake, "Waketisheni katika vikundi vya watu hamsini hamsini." 15 Wanafunzi wakafanya hivyo, wakawaketisha wote. 16 Isa akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama mbinguni, akavibariki na kuvimega. Kisha akawapa wanafunzi ili wawagawie watu. 17 Wote wakala, wakashiba. Nao wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu kumi na viwili.

Veja também