Gharama ya kumfuata Isa
57 Walipokuwa njiani wakienda, mtu mmoja akamwambia Isa, "Nitakufuata popote utakakoenda."
58 Isa akamjibu, "Mbweha wana mapango, nao ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana mahali pa kulaza kichwa chake."
59 Isa akamwambia mtu mwingine, "Nifuate."
Mtu huyo akamjibu, "Bwana9:59 Wale ambao hawakumfahamu Isa kuwa Masihi walimwita "Bwana" kwa heshima ya kawaida., niruhusu kwanza nikamzike baba yangu."
60 Isa akamwambia, "Waache wafu wawazike wafu wao, bali wewe nenda ukautangaze ufalme wa Mungu."
61 Mtu mwingine akamwambia, "Bwana, nitakufuata lakini naomba kwanza nikawaage jamaa zangu."
62 Isa akamwambia, "Mtu yeyote ashikaye jembe kulima kisha akatazama nyuma hafai kwa ufalme wa Mungu."