3 Ndipo baadhi ya watu wakaja wakamletea Isa mtu aliyepooza, akiwa amebebwa na watu wanne. 4 Kwa kuwa hawakuweza kumfikisha kwa Isa kwa sababu ya umati wa watu, walitoboa tundu kwenye paa juu ya mahali Isa alikuwa, wakamshusha mtu aliyepooza akiwa amelalia mkeka wake. 5 Isa alipoiona imani yao, alimwambia yule mtu aliyepooza, "Mwanangu, dhambi zako zimesamehewa."
6 Basi baadhi ya walimu wa Torati waliokuwa wameketi pale wakawaza mioyoni mwao, 7 "Kwa nini mtu huyu anasema hivi? Huyu anakufuru! Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake?"
8 Mara moja Isa akatambua rohoni mwake kile walichokuwa wanawaza mioyoni mwao, naye akawaambia, "Kwa nini mnawaza hivyo mioyoni mwenu? 9 Je, ni lipi lililo rahisi zaidi: kumwambia huyu aliyepooza, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Inuka, uchukue mkeka wako, uende’? 10 Lakini ili mpate kujua kwamba Mwana wa Adamu anayo mamlaka duniani ya kusamehe dhambi": Isa akamwambia yule aliyepooza, 11 "Nakuambia, inuka, chukua mkeka wako, uende nyumbani kwako." 12 Yule mtu aliyekuwa amepooza akasimama, akachukua mkeka wake, akatembea machoni pao wote! Jambo hili likawashangaza wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, "Hatujapata kuona jambo kama hili kamwe!"