Isa amponya mtu aliyepooza mkono
1 Isa akaingia tena ndani ya sinagogi3:1 Nyumba ya ibada na mafunzo., na kulikuwa na mtu aliyepooza mkono. 2 Wakawa wanamwangalia waone kama atamponya huyo mtu siku ya Sabato, ili wapate sababu ya kumshtaki. 3 Isa akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, "Njoo hapa mbele ya watu wote."
4 Kisha Isa akawauliza, "Je, ni lipi lililo halali siku ya Sabato: Ni kutenda mema au kutenda mabaya? Ni kuokoa maisha au kuua?" Lakini wao wakanyamaza.
5 Isa akawatazama kwa hasira watu waliomzunguka pande zote, akahuzunika sana kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao. Akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, "Nyoosha mkono wako." Akaunyoosha, nao ukawa umeponywa kabisa!