Pular para o conteúdo
Publicidade

Marko 5

Isa amponya mtu mwenye pepo mchafu

1 Isa na wanafunzi wake wakafika upande wa pili wa ziwa, wakaingia katika nchi ya Wagerasi. 2 Isa alipotoka kwenye mashua, mara mtu mmoja mwenye pepo mchafu akatoka makaburini, akakutana naye. 3 Mtu huyu aliishi makaburini, wala hakuna aliyeweza kumzuia hata kwa kumfunga minyororo. 4 Kwa kuwa mara kwa mara alikuwa amefungwa minyororo mikononi na miguuni, lakini akaikata hiyo minyororo na kuzivunja zile pingu miguuni mwake. Hapakuwa na mtu yeyote aliyekuwa na nguvu za kumzuia. 5 Usiku na mchana alikuwa makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikatakata kwa mawe.

6 Alipomwona Isa kwa mbali, alimkimbilia, akapiga magoti mbele yake. 7 Akapaza sauti kwa nguvu akisema, "Una nini nami, Isa, Mwana wa Mungu5:7 Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yohana 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili. Aliye Juu Sana? Ninakusihi kwa jina la Mungu, usinitese!" 8 Kwa kuwa Isa alikuwa amemwambia, "Mtoke mtu huyu, wewe pepo mchafu!"

9 Isa akamuuliza, "Jina lako ni nani?"

Akamjibu, "Jina langu ni Legioni5:9 maana yake Jeshi, kwa kuwa tuko wengi." 10 Akamsihi Isa sana asiwapeleke nje ya nchi ile.

11 Palikuwa na kundi kubwa la nguruwe lililokuwa likilisha karibu kando ya kilima. 12 Wale pepo wachafu wakamsihi Isa wakisema, "Tuamuru twende kwenye wale nguruwe. Turuhusu tuwaingie." 13 Basi Isa akawaruhusu, nao wale pepo wachafu wakatoka, wakawaingia hao nguruwe. Lile kundi lilikuwa na nguruwe wapatao elfu mbili, nao wote wakateremkia gengeni kwa kasi, nao wakatumbukia ziwani na kuzama.

14 Wale watu waliokuwa wakichunga hao nguruwe wakakimbilia mjini na vijijini kueleza yaliyotukia. Watu wakaenda kuona hayo yaliyokuwa yametukia. 15 Walipofika kwa Isa, wakamwona yule mtu aliyekuwa amepagawa na legioni ya pepo wachafu akiwa ameketi hapo, amevaa nguo na mwenye akili timamu. Wakaogopa. 16 Wale walioyaona mambo hayo wakawaeleza watu wengine yaliyomtokea yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu, na habari za lile kundi la nguruwe pia. 17 Basi watu wakaanza kumwomba Isa aondoke katika nchi yao.

18 Isa alipokuwa anaingia kwenye mashua, yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu akamsihi Isa waende pamoja. 19 Isa hakumruhusu, bali alimwambia, "Nenda nyumbani kwa jamaa yako ukawaeleze mambo makuu aliyokutendea Mwenyezi Mungu, na jinsi alivyokuhurumia." 20 Yule mtu akaenda zake, akaanza kutangaza katika Dekapoli mambo makuu Isa aliyomtendea. Nao watu wote wakastaajabu.

Veja também