Isa alisha wanaume 5,000
30 Wale mitume wakakusanyika kwa Isa na kumpa taarifa ya mambo yote waliyokuwa wamefanya na kufundisha. 31 Basi kwa kuwa watu wengi mno walikuwa wakija na kutoka, hata wakawa hawana nafasi ya kula, Isa akawaambia wanafunzi wake, "Twendeni peke yetu mahali pa faragha, mpate kupumzika."
32 Hivyo wakaondoka kwa mashua peke yao, wakaenda mahali pasipo na watu. 33 Lakini watu wengi waliowaona wakiondoka, wakawatambua, nao wakaenda haraka kwa miguu kutoka miji yote, nao wakatangulia kufika. 34 Isa alipofika kando ya bahari, aliona kundi kubwa la watu, akawahurumia kwa maana walikuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji. Kwa hiyo akaanza kuwafundisha mambo mengi.
35 Mchana ulipokuwa umeendelea sana, wanafunzi wake walienda kwake, wakamwambia, "Mahali hapa ni nyikani, nazo saa zimeenda sana. 36 Waage watu ili waende mashambani na vijijini jirani, wakajinunulie chakula."
37 Lakini Isa akawajibu, "Ninyi wapeni chakula."
Wakamwambia, "Je, twende tukanunue mikate ya dinari mia mbili6:37 Dinari moja ilikuwa kama mshahara wa kibarua wa siku moja. ili tuwape watu hawa wale?"
38 Akawauliza, "Kuna mikate mingapi? Nendeni mkaangalie."
Walipokwisha kujua, wakarudi, wakamwambia, "Kuna mikate mitano na samaki wawili."
39 Kisha Isa akawaamuru wawaketishe watu makundi makundi kwenye majani, 40 nao wakaketi kwenye vikundi vya watu mia mia, na wengine hamsini hamsini. 41 Isa akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akainua macho yake akatazama mbinguni, akavibariki na kuimega ile mikate. Kisha akawapa wanafunzi wake ili wawagawie wale watu wote. Pia akawagawia wote wale samaki wawili. 42 Watu wote wakala, wakashiba. 43 Nao wanafunzi wake wakakusanya vipande vilivyosalia vya mikate na samaki, wakajaza vikapu kumi na viwili. 44 Idadi ya wanaume waliokula walikuwa elfu tano.