Isa alisha wanaume 4,000
1 Katika siku hizo, umati mkubwa wa watu walikusanyika tena. Kwa kuwa walikuwa hawana chakula, Isa akawaita wanafunzi wake akawaambia, 2 "Ninahurumia umati huu wa watu, kwa sababu sasa wamekuwa nami kwa muda wa siku tatu na hawana chakula. 3 Nikiwaaga waende nyumbani bila kula, watazimia njiani kwa sababu baadhi yao wametoka mbali."
4 Wanafunzi wake wakamjibu, "Lakini hapa nyikani tutapata wapi mikate ya kutosha kuwalisha?"
5 Isa akawauliza, "Mna mikate mingapi?"
Wakajibu, "Tuna mikate saba."
6 Akawaambia watu waketi chini. Akaichukua ile mikate saba na kushukuru, baadaye akaimega na kuwapa wanafunzi wake ili wawagawie watu. Wanafunzi wake wakafanya hivyo. 7 Walikuwa pia na visamaki vichache, Isa akavibariki, akawaamuru wanafunzi wake wawagawie watu. 8 Wale watu walikula na kutosheka. Baadaye wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu saba. 9 Watu waliokula walikuwa wapata elfu nne. Baada ya kuwaaga,