36 Kisha Isa akaagana na ule umati, akaingia nyumbani. Wanafunzi wake wakamjia wakamwambia, "Tueleze maana ya ule mfano wa magugu shambani."
37 Akawaambia, "Aliyepanda mbegu nzuri ni Mwana wa Adamu. 38 Shamba ni ulimwengu na mbegu nzuri ni wana wa ufalme. Magugu ni wana wa yule mwovu. 39 Yule adui aliyepanda magugu ni ibilisi. Mavuno ni mwisho wa dunia, nao wavunaji ni malaika.
40 "Kama vile magugu yang’olewavyo na kuchomwa motoni, ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. 41 Mwana wa Adamu atawatuma malaika wake, nao watakusanya kutoka ufalme wake kila kitu kinachosababisha dhambi na watenda maovu wote. 42 Nao watawatupa katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno. 43 Ndipo wenye haki watang’aa kama jua katika ufalme wa Baba13:43 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. yao. Yeye aliye na masikio, na asikie.