15 Ilipofika jioni, wanafunzi wake walienda kwake, wakamwambia, "Mahali hapa ni nyikani, na muda sasa umekwisha. Waage makundi ya watu ili waende zao vijijini wakajinunulie chakula."
16 Isa akawaambia, "Hakuna sababu ya wao kuondoka. Ninyi wapeni chakula."
17 Wakamjibu, "Tuna mikate mitano na samaki wawili tu."
18 Akawaambia, "Nileteeni hivyo vitu hapa." 19 Isa akaagiza umati wa watu wakae chini kwenye nyasi. Akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akainua macho yake akatazama mbinguni, akavibariki na kuimega ile mikate. Kisha akawapa wanafunzi, nao wanafunzi wakawagawia ule umati. 20 Wote wakala, wakashiba. Nao wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu kumi na viwili. 21 Idadi ya watu waliokula walikuwa wanaume wapatao elfu tano, bila kuhesabu wanawake na watoto.