Isa aingia Yerusalemu kwa shangwe
1 Walipokaribia Yerusalemu, wakafika Bethfage katika Mlima wa Mizeituni. Ndipo Isa akawatuma wanafunzi wake wawili, 2 akawaambia, "Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu, nanyi mtampata punda amefungwa hapo, na mwana-punda pamoja naye. Wafungueni na mniletee. 3 Mtu yeyote akiwasemesha lolote, mwambieni kwamba Bwana ana haja nao, naye atawaruhusu mwalete mara moja."
4 Haya yalitukia ili litimie neno lililonenwa na nabii, aliposema:
5 "Mwambieni Binti Sayuni,
‘Tazama, mfalme wako anakuja kwako,
ni mpole, naye amepanda punda,
juu ya mwana-punda, mtoto wa punda.’ "
6 Wale wanafunzi wakaenda, wakafanya kama Isa alivyokuwa amewaagiza. 7 Wakamleta yule punda na mwana-punda, nao wakatandika mavazi yao juu ya hao punda, naye Isa akaketi juu yake. 8 Umati mkubwa wa watu wakatandaza mavazi yao barabarani, na wengine wakakata matawi kwenye miti, wakayatandaza barabarani. 9 Wale umati wa watu waliomtangulia na wale waliomfuata wakapaza sauti na kusema,
"Hosana21:9 Kiebrania kusema Okoa; basi likawa neno la shangwe., Mwana wa Daudi!"
"Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Mwenyezi Mungu!"
"Hosana juu mbinguni!"
10 Isa alipoingia Yerusalemu, mji wote ukataharuki, watu wakauliza, "Huyu ni nani?"
11 Wale umati wa watu wakajibu, "Huyu ni Isa, yule nabii kutoka Nasiri ya Galilaya."