Isa amponya mwanamke na kumfufua msichana
18 Isa alipokuwa akiwaambia mambo haya, kiongozi wa sinagogi9:18 Nyumba ya ibada na mafunzo. akaingia, akapiga magoti mbele yake, akamwambia, "Binti yangu amekufa sasa hivi. Lakini njoo uweke mkono wako juu yake, naye ataishi." 19 Isa akaondoka akafuatana naye, nao wanafunzi wake pia wakaandamana naye.
20 Wakati huo huo, mwanamke mmoja, aliyekuwa na ugonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na mbili, akaja nyuma ya Isa, akagusa upindo wa vazi lake, 21 kwa maana alisema moyoni mwake, "Nikigusa tu vazi lake, nitaponywa."
22 Isa akageuka, naye alipomwona akamwambia, "Binti, jipe moyo, imani yako imekuponya." Naye yule mwanamke akapona kuanzia saa hiyo.
23 Isa alipofika nyumbani mwa yule kiongozi wa sinagogi na kuwaona waombolezaji wakipiga filimbi za maombolezo na watu wengi wakipiga kelele, 24 akawaambia, "Ondokeni! Kwa maana binti huyu hakufa, bali amelala." Wakamcheka kwa dhihaka. 25 Lakini watu walipokwisha kutolewa nje, akaingia mle ndani na kumshika yule binti mkono, naye akaamka. 26 Habari hizi zikaenea katika maeneo yale yote.