2 Wakati huo huo wakamletea mtu aliyepooza, akiwa amelazwa kwenye mkeka. Isa alipoiona imani yao, alimwambia yule mtu aliyepooza, "Mwanangu, jipe moyo mkuu. Dhambi zako zimesamehewa."
3 Kwa ajili ya jambo hili, baadhi ya walimu wa Torati wakasema mioyoni mwao, "Huyu mtu anakufuru!"
4 Lakini Isa akiyafahamu mawazo yao, akawaambia, "Kwa nini mnawaza maovu mioyoni mwenu? 5 Je, ni lipi lililo rahisi zaidi: kusema, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Inuka, uende’? 6 Lakini nataka mpate kujua kwamba Mwana wa Adamu ana mamlaka duniani kusamehe dhambi." Ndipo akamwambia yule aliyepooza, "Inuka, chukua mkeka wako, uende nyumbani mwako." 7 Yule mtu akasimama, akaenda nyumbani mwake.