Nehemia akagua kuta za Yerusalemu
11 Nilienda Yerusalemu, na baada ya kukaa huko siku tatu, 12 nikaondoka wakati wa usiku pamoja na watu wachache. Sikuwa nimemwambia mtu yeyote kile ambacho Mungu wangu alikuwa ameweka moyoni mwangu kufanya kwa ajili ya Yerusalemu. Hapakuwa na mnyama yeyote nami isipokuwa yule niliyekuwa nimempanda.
13 Nikatoka nje usiku kupitia Lango la Bondeni, kuelekea Kisima cha Joka na Lango la Samadi, nikikagua kuta za Yerusalemu zilizokuwa zimebomolewa, na malango yake yaliyokuwa yameteketezwa kwa moto. 14 Kisha nikaelekea hadi Lango la Chemchemi na Bwawa la Mfalme, lakini hapakuwa na nafasi ya kutosha mnyama wangu kupita, 15 kwa hiyo nikapandia bondeni usiku nikikagua ukuta. Mwishoni nikarudi na kuingia tena kupitia Lango la Bondeni. 16 Maafisa hawakujua nilikoenda wala nilichokuwa nikifanya, kwa sababu nilikuwa bado sijasema lolote kwa Wayahudi, wala makuhani, wala wakuu, wala maafisa, wala mtu yeyote ambaye angefanya kazi.