Siku kubwa ya Mwenyezi Mungu
14 "Siku kubwa ya Mwenyezi Mungu iko karibu:
iko karibu na inakuja haraka.
Sikilizeni! Kilio katika siku ya Mwenyezi Mungu
kitakuwa chungu.
Shujaa atapiga ukelele wa vita huko.
15 Siku ile ni siku ya ghadhabu,
siku ya fadhaa na dhiki,
siku ya uharibifu na ukiwa,
siku ya giza na utusitusi,
siku ya mawingu na giza nene,
16 siku ya tarumbeta na kelele za vita
dhidi ya miji yenye ngome,
na dhidi ya minara mirefu.
17 Nitawaletea watu dhiki,
nao watatembea kama vipofu,
kwa sababu wametenda dhambi
dhidi ya Mwenyezi Mungu.
Damu yao itamwagwa kama vumbi
na matumbo yao kama kinyesi.
18 Fedha yao wala dhahabu yao
hazitaweza kuwaokoa
katika siku hiyo ya ghadhabu ya Mwenyezi Mungu.
Katika moto wa wivu wake
dunia yote itateketezwa,
kwa maana ghafula ataleta mwisho
wa wote wanaoishi duniani."