11 Kwa maana neema ya Mungu ambayo inawaokoa wanadamu wote imefunuliwa. 12 Nayo inatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia, ili tupate kuishi maisha ya kiasi, ya haki na ya utaua katika ulimwengu huu wa sasa, 13 huku tukilitazamia tumaini lenye baraka na ufunuo wa utukufu wa Mungu wetu Mkuu, aliye Mwokozi wetu Isa Al-Masihi. 14 Ndiye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe kutoka uovu wote na kujisafishia watu kuwa mali yake Mwenyewe, yaani wale walio na juhudi katika kutenda mema.