1 Mt 10:16;Ufu 12:2,9;20:2 Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya BWANA Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani? 2 Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula; 3 Mwa 2:16,17 lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa. 4 2 Kor 11:3;1 Tim 2:14 Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa, 5 kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya. 6 Rum 5:12-19 Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alichuma matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala. 7 Wakafumbuliwa macho wote wawili wakajitambua kuwa wako uchi, wakashona majani ya mtini, na kujifanyia mavazi ya kusitiri uchi wao. 8 Ayu 31:33;38:1;Zab 139:1-12;Yer 23:34;Amo 9:3 Kisha wakasikia sauti ya BWANA Mungu, akitembea bustanini wakati wa jua kupunga; Adamu na mkewe wakajificha kati ya miti ya bustani, BWANA Mungu asiwaone. 9 Mwa 4:9 BWANA Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? 10 Ayu 23:15;1 Yoh 3:20 Akasema, Nilisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha. 11 Akasema, Ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi? Je! Umekula matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? 12 Mit 28:13;Yak 1:13 Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala. 13 2 Kor 11:3;1 Tim 2:14 BWANA Mungu akamwambia mwanamke, Nini hili ulilolifanya? Mwanamke akasema, Nyoka alinidanganya, nikala. 14 Isa 65:25;Mik 7:17 BWANA Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako; 15 Hes 21:6,7;Rum 16:20;Ebr 2:14;1 Yoh 3:8;Ufu 12:17 nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino. 16 Yn 16:21;1 Tim 2:15 Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa uchungu utazaa watoto; hata hivyo, hamu yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala. 17 Ayu 5:7;Mhu 2:23;Ebr 6:8 Akamwambia Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nilikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako; 18 michongoma na miiba itakuzalia, nawe utakula mboga za kondeni; 19 1 Kor 15:21,22 kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi.
20 Adamu akamwita mkewe jina lake Hawa; kwa kuwa yeye ndiye aliye mama yao wote walio hai. 21 BWANA Mungu akawafanyia Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika.
22 Mwa 3:5;2:9;Ufu 22:14 BWANA Mungu akasema, Basi, huyu mtu amekuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya; na sasa asije akanyosha mkono wake akatwaa matunda ya mti wa uzima, akala, akaishi milele; 23 kwa hiyo BWANA Mungu akamtoa katika bustani ya Edeni, ailime ardhi ambayo katika hiyo alitwaliwa. 24 Mwa 2:8;Zab 104:4;Ebr 1:7;Yn 14:6 Basi akamfukuza huyo mtu, akaweka Makerubi, upande wa mashariki wa bustani ya Edeni, na upanga wa moto uliogeuka huku na huko, kuilinda njia ya mti wa uzima.