Publicidade

Lamentações 1

Mji uliohamwa

1 Jinsi mji huu ukaavyo ukiwa,

Huo uliokuwa umejaa watu!

Jinsi alivyokuwa kama mjane,

Yeye aliyekuwa mkuu kati ya mataifa!

Binti mfalme kati ya majimbo,

Jinsi alivyoshikwa shokoa!

2 Hulia sana wakati wa usiku,

Na machozi yake yapo mashavuni;

Miongoni mwa wote waliompenda

Hakuna hata mmoja amfarijiye;

Rafiki zake wote wamemtenda hila,

Wamekuwa adui zake.

3 Yuda amehamishwa kwa sababu ya kuonewa,

Na kwa sababu ya utumwa mkuu;

Anakaa kati ya mataifa,

Haoni raha yoyote;

Wote waliomfuata wamempata

Katika dhiki yake.

4 Njia za Sayuni zaomboleza,

Kwa kuwa hakuna ajaye kwa sikukuu;

Malango yake yote yamekuwa ukiwa,

Makuhani wake hupiga kite;

Wanawali wake wanahuzunika;

Na yeye mwenyewe huona uchungu.

5 Watesi wake wamekuwa kichwa,

Adui zake hufanikiwa;

Kwa kuwa BWANA amemtesa

Kwa sababu ya wingi wa makosa yake;

Watoto wake wadogo wamechukuliwa mateka

Mbele yake huyo mtesi.

6 Naye huyo binti Sayuni

Enzi yake yote imemwacha;

Wakuu wake wamekuwa kama ayala

Wasioona malisho;

Nao wamekwenda zao hawana nguvu

Mbele yake anayewafuatia.

7 Siku za mateso na misiba yake,

Yerusalemu huyakumbuka matamanio yake yote

Yaliyokuwa tangu siku za kale;

Hapo watu wake walipoanguka mikononi mwa mtesi,

Wala hakuna hata mmoja wa kumsaidia;

Hao watesi wake walimwona,

Wakafanya sabato zake kuwa mzaha.

8 Yerusalemu amefanya dhambi sana;

Kwa hiyo amekuwa kama kitu kichafu;

Wote waliomheshimu wanamdharau,

Kwa sababu wameuona uchi wake;

Naam, yeye anaugua,

Na kujigeuza aende nyuma.

9 Uchafu wake ulikuwa katika marinda yake;

Hakukumbuka mwisho wake;

Kwa hiyo ameshuka kwa ajabu;

Yeye hana mtu wa kumfariji;

Tazama, BWANA, mateso yangu;

Maana huyo adui amejitukuza.

10 Huyo mtesi amenyosha mkono wake

Juu ya matamanio yake yote;

Maana ameona ya kuwa mataifa wameingia

Ndani ya patakatifu pake;

Ambao kwa habari zao wewe uliamuru

Wasiingie katika kusanyiko lako.

11 Watu wake wote hupiga kite,

Wanatafuta chakula;

Wameyatoa matamanio yao wapate chakula

Cha kuihuisha nafsi;

Ee BWANA, tazama, uangalie;

Kwa maana mimi nimekuwa mnyonge.

12 Je! Si kitu kwenu, enyi nyote mpitao njia,

Angalieni, mtazame

Kama kuna majonzi yoyote mfano wa majonzi yangu,

Niliyotendwa mimi,

Ambayo BWANA amenihuzunisha kwa hayo

Siku ya hasira yake iwakayo.

13 Toka juu amepeleka moto mifupani mwangu,

Nao umeishinda;

Ametandika wavu aninase miguu,

Amenirudisha nyuma;

Amenifanya kuwa mtu wa pekee,

Na mgonjwa mchana kutwa.

14 Kongwa la makosa yangu limefungwa na mkono wake;

Hayo yameshikamana;

Yamepanda juu shingoni mwangu;

Amezikomesha nguvu zangu;

15 Bwana amenitia mikononi mwao,

Ambao siwezi kupingamana nao.

Bwana amewafanya mashujaa wangu wote

Kuwa si kitu kati yangu;

Ameita mkutano mkuu kinyume changu

Ili kuwaponda vijana wangu;

Bwana amemkanyaga kama shinikizoni

Huyo bikira binti Yuda.

16 Mimi ninayalilia mambo hayo;

Jicho langu, jicho langu linachuruzika machozi;

Kwa kuwa mfariji yuko mbali nami,

Ambaye ilimpasa kunihuisha nafsi;

Watoto wangu wameachwa peke yao,

Kwa sababu huyo adui ameshinda.

17 Sayuni huinyosha mikono yake;

Hakuna hata mmoja wa kumfariji;

BWANA ametoa amri juu ya Yakobo,

Kwamba wamzungukao wawe watesi wake;

Yerusalemu amekuwa kati yao

Kama kitu kichafu.

18 BWANA ndiye mwenye haki;

Maana nimeiasi amri yake;

Sikieni, nawasihi, enyi watu wote,

Mkayatazame majonzi yangu;

Wasichana wangu na wavulana wangu

Wamechukuliwa mateka.

19 Niliwaita hao walionipenda

Lakini walinidanganya;

Makuhani wangu na wazee wangu

Walifariki mjini;

Hapo walipokuwa wakitafuta chakula

ili kuzihuisha nafsi zao.

20 Angalia, Ee BWANA; maana mimi ni katika dhiki;

Mtima wangu umetaabika;

Moyo wangu umegeuka ndani yangu;

Maana nimeasi vibaya sana;

Huko nje upanga huua watu;

Nyumbani mna kama mauti.

21 Wamesikia kwamba napiga kite;

Hakuna hata mmoja wa kunifariji;

Adui zangu wote wamesikia habari ya mashaka yaliyonipata;

Hufurahi kwa kuwa umeyafanya hayo;

Utaileta siku ile uliyoitangaza,

Nao watakuwa kama mimi.

22 Huo uovu wao wote

Na uje mbele zako wewe;

Ukawatende wao kama ulivyonitenda mimi

Kwa dhambi zangu zote;

Kwa maana mauguzi yangu ni mengi sana,

Na moyo wangu umezimia.

Veja também

Publicidade
Lamentações
Ver todos os capítulos de Lamentações
Bíblia Online Bíblia Online

Bíblia Online • Versão: 2026-06-18_14-04-22-