1 Ee BWANA, kumbuka yaliyotupata;
Utazame na kuiona aibu yetu.
2 Urithi wetu umegeuka kuwa mali ya wageni;
Na nyumba zetu kuwa mali ya mataifa.
3 Tumekuwa yatima waliofiwa na baba;
Mama zetu wamekuwa kama wajane.
4 Tumekunywa maji yetu kwa fedha;
Kuni zetu twauziwa.
5 Watufuatiao wako juu ya shingo zetu;
Tumechoka, tusipate pumziko lolote.
6 Tumewapa hao Wamisri mkono;
Na Waashuri nao, ili tushibe chakula.
7 Baba zetu walitenda dhambi hata hawako;
Na sisi tumeyachukua maovu yao.
8 Watumwa wanatutawala;
Hakuna mtu wa kutuokoa na mikono yao.
9 Twapata chakula kwa kujihatarisha nafsi zetu;
Kwa sababu ya upanga wa nyikani.
10 Ngozi yetu ni nyeusi kama tanuri;
Kwa sababu ya joto ya njaa ituteketezayo.
11 Wanawake katika Sayuni wanashikwa kwa nguvu;
Na mabikira katika miji ya Yuda.
12 Wakuu hutundikwa kwa mikono yao;
Nyuso za wazee hazipewi heshima.
13 Vijana huyachukua mawe ya kusagia;
Na watoto hujikwaa chini ya kuni.
14 Wazee wameacha kwenda langoni;
Na vijana kwenda ngomani.
15 Furaha ya mioyo yetu imekoma;
Machezo yetu yamegeuka maombolezo.
16 Taji ya kichwa chetu imeanguka;
Ole wetu! Kwa kuwa tumetenda dhambi.
17 Kwa sababu hiyo mioyo yetu imezimia;
Kwa ajili ya hayo macho yetu hayaoni vema.
18 Kwa ajili ya mlima Sayuni ulio ukiwa,
Mbweha hutembea juu yake.
19 Wewe, BWANA, unadumu milele;
Kiti chako cha enzi ni tangu kizazi hata kizazi.
20 Mbona watusahau sikuzote;
Na kutuacha muda huu mwingi?
21 Ee BWANA, utugeuze kwako, nasi tutageuka; Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale.
22 Ingawa wewe umetukataa kabisa;
Nawe una hasira nyingi sana juu yetu.