Publicidade

Lamentações 4

Adhabu ya Sayuni

1 Jinsi dhahabu ilivyoacha kung'aa,

Na dhahabu iliyo safi ilivyobadilika!

Mawe ya patakatifu yametupwa

Mwanzo wa kila njia.

2 Wana wa Sayuni wenye thamani,

Walinganao na dhahabu safi,

Jinsi wanavyodhaniwa kuwa vyombo vya udongo,

Kazi ya mikono ya mfinyanzi!

3 Hata mbwamwitu hutoa matiti,

Huwanyonyesha watoto wao;

Binti ya watu wangu amekuwa mkali,

Mfano wa mbuni jangwani.

4 Ulimi wa mtoto anyonyaye

Wagandamana na kinywa chake kwa kiu;

Watoto wachanga waomba chakula,

Wala hakuna hata mmoja awamegeaye.

5 Wale waliokula vitu vya anasa

Wameachwa peke yao njiani;

Wale waliokuzwa kuvaa nguo nyekundu

Wakumbatia jaa.

6 Maana uovu wa binti ya watu wangu ni mkubwa

Kuliko dhambi ya Sodoma,

Uliopinduliwa kama katika dakika moja,

Wala mikono haikuwekwa juu yake.

7 Wakuu wake walikuwa safi kuliko theluji,

Walikuwa weupe kuliko maziwa;

Miili yao, walikuwa wekundu kuliko marijani,

Na umbo lao kama yakuti samawi.

8 Nyuso zao ni nyeusi kuliko makaa;

Hawajulikani katika njia kuu;

Ngozi yao yagandamana na mifupa yao

Imekauka, imekuwa kama mti.

9 Heri wale waliouawa kwa upanga

Kuliko wao waliouawa kwa njaa;

Maana hao husinyaa, wakichomwa

Kwa kukosa matunda ya mashamba.

10 Mikono ya wanawake wenye huruma

Imewatokosa watoto wao wenyewe;

Walikuwa ndio chakula chao

Katika uharibifu wa binti ya watu wangu.

11 BWANA ameitimiza ghadhabu yake,

Ameimimina hasira yake kali;

Naye amewasha moto katika Sayuni

Ulioiteketeza misingi yake.

12 Wafalme wa dunia hawakusadiki,

Wala wote wakaao duniani,

Ya kwamba mtesi na adui wangeingia

Katika malango ya Yerusalemu.

13 Ni kwa sababu ya dhambi za manabii wake

Na maovu ya makuhani wake,

Walioimwaga damu ya wenye haki

Katikati yake.

14 Hutangatanga njiani kama vipofu,

Wametiwa unajisi kwa damu;

Hata ikawa hakuna aliyeweza

Kuyagusa mavazi yao.

15 Watu waliwapigia kelele, Ondokeni, Uchafu,

Ondokeni, ondokeni, msiguse;

Walipokimbia na kutangatanga, watu walisema kati ya mataifa,

Hawatakaa hapa tena.

16 Hasira ya BWANA imewatenga,

Yeye hatawaangalia tena;

Hawakujali nafsi za wale makuhani,

Hawakuwaheshimu wazee wao.

17 Macho yetu yamechoka

Kwa kuutazamia bure msaada wetu;

Katika kungoja kwetu tumengojea taifa

Lisiloweza kutuokoa.

18 Wanatuvizia hatua zetu,

Hata hatuwezi kwenda katika njia zetu;

Mwisho wetu umekaribia, siku zetu zimetimia;

Maana mwisho wetu umefika.

19 Waliotufuatia ni wepesi

Kuliko tai za mbinguni;

Hao walitufuatia milimani,

Nao walituotea jangwani.

20 Pumzi ya mianzi ya pua zetu, masihi wa BWANA,

Alikamatwa katika marima yao;

Ambaye kwa habari zake tulisema,

Chini ya kivuli chake tutakaa kati ya mataifa.

21 Furahi, ushangilie, Ee binti Edomu,

Ukaaye katika nchi ya Usi;

Hata kwako kikombe kitapita,

Utalewa, na kujifanya uchi.

22 Adhabu ya uovu wako imetimia, Ee binti Sayuni;

Hatakuhamisha tena;

Atapatiliza uovu wako, Ee binti Edomu;

Atazivumbua dhambi zako.

Veja também

Publicidade
Lamentações
Ver todos os capítulos de Lamentações
Bíblia Online Bíblia Online

Bíblia Online • Versão: 2026-06-16_18-40-07-