1 Jinsi Bwana alivyomfunika binti Sayuni
Kwa wingu katika hasira yake!
Ameutupa toka mbinguni hata nchi
Huo uzuri wa Israeli;
Wala hakukikumbuka kiti cha miguu yake
Katika siku ya hasira yake.
2 Bwana ameyameza makao yote ya Yakobo,
Wala hakuona huruma;
Ameziangusha ngome za binti Yuda
Katika ghadhabu yake;
Amezibomoa hata nchi
Ameunajisi ufalme na wakuu wake.
3 Ameikata pembe yote ya Israeli
Katika hasira yake kali;
Ameurudisha nyuma mkono wake wa kulia
Mbele ya hao adui,
Naye amemteketeza Yakobo kama moto uwakao,
Ulao pande zote.
4 Ameupinda upinde wake kama adui,
Amesimama na mkono wake wa kulia kama mtesi;
Naye amewaua hao wote
Waliopendeza macho;
Katika hema ya binti Sayuni
Amemimina ghadhabu yake kama moto.
5 Bwana amekuwa mfano wa adui,
Amemmeza Israeli;
Ameyameza majumba yake yote,
Ameziharibu ngome zake;
Tena amemzidishia binti Yuda
Matanga na maombolezo.
6 Naye ameondoa maskani yake kwa nguvu,
Kana kwamba ni ya bustani tu;
Ameziharibu sikukuu zake;
BWANA amezisahaulisha katika Sayuni
Sikukuu na sabato;
Naye amewadharau mfalme na kuhani
Katika uchungu wa hasira yake.
7 Bwana ameitupilia mbali madhabahu yake,
Amepachukia patakatifu pake;
Amezitia katika mikono ya hao adui
Kuta za majumba yake;
Wamepiga kelele ndani ya nyumba ya BWANA
Kama katika sikukuu.
8 BWANA amekusudia kuuharibu
Ukuta wa binti Sayuni;
Ameinyosha hiyo kamba,
Hakuuzuia mkono wake usiangamize;
Bali amefanya boma na ukuta kuomboleza;
Zote pamoja hudhoofika.
9 Malango yake yamezama katika nchi;
Ameyaharibu makomeo yake na kuyavunja;
Mfalme wake na wakuu wake wanakaa
Kati ya mataifa wasio na sheria;
Naam, manabii wake hawapati maono
Yatokayo kwa BWANA.
10 Wazee wa binti Sayuni huketi chini,
Hunyamaza kimya;
Wametupa mavumbi juu ya vichwa vyao,
Wamejivika viunoni nguo za magunia;
Wanawali wa Yerusalemu huinama vichwa vyao
Kuielekea nchi.
11 Macho yangu yamechoka kwa machozi,
Mtima wangu umetaabika;
Ini langu linamiminwa juu ya nchi
Kwa uharibifu wa binti ya watu wangu;
Kwa sababu watoto wachanga na wanyonyao,
Huzimia katika mitaa ya mji.
12 Wao huwauliza mama zao,
Ziko wapi nafaka na divai?
Hapo wazimiapo kama waliojeruhiwa
Katika mitaa ya mji,
Hapo walipomiminika nafsi zao
Vifuani mwa mama zao.
13 Nikushuhudie nini? Nikufananishe na nini,
Ee Binti Yerusalemu?
Nikulinganishe na nini, nipate kukufariji,
Ee bikira binti Sayuni?
Kwa maana uvunjifu wako ni mkuu kama bahari,
Ni nani awezaye kukuponya?
14 Manabii wako wameona maono kwa ajili yako
Ya ubatili na upumbavu
Wala hawakufunua uovu wako,
Wapate kurudisha kufungwa kwako;
Bali wameona mabashiri ya ubatili kwa ajili yako
Na sababu za kuhamishwa.
15 Hao watu wote wapitao
Hukupigia makofi;
Humzomea binti Yerusalemu,
Na kutikisa vichwa vyao;
Je! Mji huu ndio ulioitwa, Ukamilifu wa uzuri,
Furaha ya dunia yote?
16 Juu yako adui zako wote
Wamepanua vinywa vyao;
Huzomea, husaga meno yao,
Husema, Tumemmeza;
Hakika siku hii ndiyo tuliyoitazamia;
Tumeipata, tumeiona.
17 BWANA ameyatenda aliyoyakusudia; amelitimiza neno lake,
Aliloliamuru siku za kale;
Ameangusha hata chini,
Wala hakuona huruma;
Naye amemfurahisha adui juu yako,
Ameitukuza pembe ya watesi wako.
18 Mioyo yao ilimlilia Bwana;
Ee ukuta wa binti Sayuni!
Machozi na yachuruzike kama mto
Mchana na usiku;
Usijipatie kupumzika;
Mboni ya jicho lako isikome.
19 Inuka, ulalamike usiku,
Mwanzo wa mikesha yake;
Mimina moyo wako kama maji usoni pa Bwana;
Umwinulie mikono yako;
Kwa uhai wa watoto wako wachanga wazimiao kwa njaa,
Mwanzo wa kila njia kuu.
20 Tazama, BWANA, uangalie,
Ni nani uliyemtenda hayo!
Je! Wanawake wale mazao yao,
Watoto waliowabeba?
Je! Kuhani na nabii wauawe
Katika patakatifu pa Bwana?
21 Kijana na mzee hulala chini
Katika njia kuu;
Wasichana wangu na wavulana wangu
Wameanguka kwa upanga;
Umewaua katika siku ya hasira yako;
Umeua, wala hukuona huruma.
22 Umeziita kama katika siku ya mkutano wa makini;
Hofu zangu zije pande zote;
Wala hapana hata mmoja aliyepona wala kusalia
Katika siku ya hasira ya BWANA;
Hao niliowabeba na kuwalea
Huyo adui yangu amewakomesha.