Yesu aingia Yerusalemu kwa shangwe
1 Mk 11:1-10;Lk 19:29-38;Yn 12:12-19Walipokaribia Yerusalemu, na kufika Bethfage, katika mlima wa Mizeituni, ndipo Yesu alipotuma wanafunzi wawili akiwaambia, 2 Nendeni katika kijiji kile kinachowakabili, na mara mtaona punda amefungwa, na mwanapunda pamoja naye; wafungueni mniletee. 3 Mt 26:18Na kama mtu akiwaambia neno, semeni, Bwana anawahitaji; naye atawatuma mara moja. 4 Haya yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema,
5 Zek 9:9;Isa 62:11Mwambieni binti Sayuni
Tazama, mfalme wako anakuja kwako,
Mpole, naye amepanda punda,
Na mwanapunda, mtoto wa punda.
6 Wale wanafunzi wakaenda zao, wakafanya kama Yesu alivyowaamuru, 7 wakamleta yule punda na mwanapunda, wakaweka nguo zao juu yao, naye akaketi juu yake. 8 2 Fal 9:13Watu wengi katika ule mkutano wakatandaza nguo zao njiani; na wengine wakakata matawi ya miti, wakayatandaza njiani. 9 Zab 118:25-26;2 Sam 14:4Na makutano waliotangulia, na wale waliofuata, wakapaza sauti, wakisema, Hosana, Mwana wa Daudi; ndiye mbarikiwa, yeye ajaye kwa jina la Bwana; Hosana juu mbinguni. 10 Hata alipoingia Yerusalemu, mji wote ukataharuki, watu wakisema, Ni nani huyu? 11 Mt 21:46Makutano wakasema, Huyu ni yule nabii, Yesu, wa Nazareti ya Galilaya.