Publicidade

Êxodo 23

Haki kwa wote

1 Usivumishe habari za uongo; usishirikiane na mwovu kwa kuwa shahidi wa uongo. 2 Usiwafuate walio wengi kutenda uovu; wala usitie ushahidi wako katika neno lolote kwa kugeukia kando na kuandamana na mkutano ili kupotoa hukumu; 3 wala usimpendelee mtu mnyonge katika neno lake. 4 Ukimwona ng'ombe wa adui wako, au punda wake, amepotea, sharti umrudishie mwenyewe tena. 5 Ukimwona punda wake huyo akuchukiaye akiwa ameanguka chini ya mzigo wake, na wewe ungejizuia usimsaidie, lazima umsaidie.

6 Usipotoe hukumu ya mtu maskini katika neno lake. 7 Jitenge mbali na neno la uongo; wala wasio hatia na wenye haki usiwaue; kwa kuwa mimi sitamhesabia haki yeye aliye mwovu. 8 Nawe usipokee rushwa; kwani hiyo rushwa huwapofusha macho hao waonao, na kuyapotoa maneno ya wenye haki. 9 Usimwonee mgeni; maana, ninyi mwajua moyo wa mgeni ulivyo, kwa kuwa ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri.

Sheria kuhusu mwaka wa saba na Sabato

10 Utapanda mbegu katika nchi yako muda wa miaka sita na kupata mavuno yake; 11 lakini mwaka wa saba utaiacha nchi ipumzike na kutulia; hao maskini miongoni mwa watu wako wapate kula; na hicho watakachosaza wao, wapate kula wanyama wa kondeni. Utafanya vivyo hivyo katika shamba lako la mizabibu, na katika shamba lako la mizeituni. 12 Siku sita utafanya kazi yako, na siku ya saba utapumzika; ili kwamba ng'ombe wako na punda wako wapate kupumzika, kisha mwana wa mjakazi wako na mgeni wapate kuburudika. 13 Yaangalieni hayo yote niliyowaambia; wala msitaje kabisa majina ya miungu mingine, wala yasisikizwe kutoka kinywani mwako.

Sikukuu za kila mwaka

14 Mara tatu kila mwaka utaniwekea sikukuu. 15 Utaiweka sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu; utakula mikate isiyochachwa muda wa siku saba kama nilivyokuagiza, kwa wakati uliowekwa, mwezi wa Abibu (kwa maana ndio mwezi uliotoka Misri); wala hapana mtu atakayeonekana mbele yangu na mikono mitupu; 16 tena, sikukuu ya mavuno, hayo malimbuko ya kazi zako za kupanda mashambani; tena, sikukuu ya kukusanya, mwisho wa mwaka, hapo utakapokusanya hayo uliyoyataabikia shambani. 17 Mara tatu katika mwaka wana wa kiume wako wote watahudhuria mbele ya Bwana MUNGU.

18 Usinitolee damu ya dhabihu zangu pamoja na mkate uliotiwa chachu, wala mafuta ya sikukuu yangu usiyaache kusalia hadi asubuhi. 19 Ya kwanza ya malimbuko ya nchi yako utayaleta na kuyatia ndani ya nyumba ya BWANA, Mungu wako. Usimtokose mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake.

Kuahidiwa Ushindi juu ya Kanaani

20 Tazama, mimi namtuma malaika aende mbele yako, ili akulinde njiani na kukupeleka mpaka mahali pale nilipokuandalia. 21 Jitunzeni mbele yake, muisikize sauti yake; wala msimtie kasirani; maana, hatawasamehe makosa yenu; kwa kuwa jina langu limo ndani yake. 22 Lakini ukiisikiza sauti yake kweli, na kuyatenda yote ninenayo mimi; ndipo mimi nitakuwa ni adui wa adui zako, na mtesi wa hao wakutesao. 23 Kwa kuwa malaika wangu atatangulia mbele yako, na kukufikisha kwa Mwamori, na Mhiti, na Mperizi, na Mkanaani, na Mhivi, na Myebusi; nami nitawatupilia mbali. 24 Usiisujudie miungu yao, wala kuitumikia; wala usitende mfano wa matendo yao; bali utaiangamiza kabisa, na nguzo zao utazivunja vipande vipande. 25 Nanyi mtamtumikia BWANA, Mungu wenu, naye atakibarikia chakula chako, na maji yako; nami nitakuondolea ugonjwa kati yako. 26 Hapatakuwa na mwenye kuharibu mimba, wala aliye tasa, katika nchi yako; na hesabu ya siku zako nitaitimiza. 27 Nitatuma utisho wangu utangulie mbele yako, nami nitawafadhaisha watu wote utakaowafikia, nami nitawafanya hao adui zako wote wakuoneshe maungo yao. 28 Nami nitapeleka mavu mbele yako, watakaomfukuza Mhivi, na Mkanaani, na Mhiti, watoke mbele yako. 29 Sitawafukuza mbele yako katika mwaka mmoja; nchi isiwe ukiwa, na wanyama wa pori wakaongezeka na kukusumbua. 30 Nitawafukuza kidogo kidogo mbele yako, hata utakapoongezeka wewe, na kuirithi hiyo nchi. 31 Nami nitakuwekea mpaka wako tangu Bahari ya Shamu hadi bahari ya Wafilisti, tena tangu jangwani hata huo Mto; kwa kuwa nitawatia wenyeji wa nchi mkononi mwako; nawe utawafukuza mbele yako. 32 Usifanye maagano pamoja nao, wala pamoja na miungu yao. 33 Wasikae katika nchi yako, wasije wakakufanya kunitendea mimi dhambi; kwa sababu ukiitumikia miungu yao, jambo hili halikosi litakuwa ni (mtego) tanzi kwako.

Veja também

Publicidade
Bíblia Online Bíblia Online

Bíblia Online • Versão: 2026-06-16_18-40-07-