Mungu ailaumu Israeli
1 Mik 6:2;Yer 4:22 Lisikieni neno la BWANA, enyi wana wa Israeli; kwa maana BWANA ana shutuma nao wakaao katika nchi, kwa sababu hapana kweli, wala fadhili, wala kumjua Mungu katika nchi. 2 Hapana neno ila kuapa kwa uongo, na kuvunja ahadi, na kuua, na kuiba, na kuzini; huruka mpaka, na kumwaga damu mfululizo. 3 Amo 8:8;Sef 1:3 Kwa ajili ya hayo nchi itaomboleza, na kila mtu akaaye ndani yake atadhoofika, pamoja na wanyama wa porini na ndege wa angani; naam, samaki wa baharini pia wataangamizwa.
4 Kum 17:12 Lakini asishindane mtu, wala mtu asikemee; maana watu wako ni kama wao washindanao na kuhani. 5 Yer 6:4 Na wewe utajikwaa wakati wa mchana, na nabii naye atajikwaa pamoja nawe wakati wa usiku; nami nitamwangamiza mama yako. 6 Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi nami nitawasahau watoto wako. 7 Kadiri walivyozidishwa, kwa kadiri iyo hiyo walinitenda dhambi; nami nitageuza utukufu wao kuwa aibu. 8 Hujilisha dhambi ya watu wangu, hujifurahisha moyo kwa uovu wao. 9 Hata itakuwa, kama walivyo watu, ndivyo atakavyokuwa kuhani; nami nitawaadhibu kwa ajili ya njia zao, na kuwalipa kwa matendo yao.
10 Mik 6:14;Hag 1:6 Nao watakula, lakini hawatashiba; watafanya zinaa, lakini hawataongezeka; kwa sababu wameacha kumwangalia BWANA.
Uzinzi wa Israeli
11 Isa 28:7 Uzinzi na divai mpya huondoa fahamu za wanadamu. 12 Yer 2:27;Isa 44:20;Ufu 17:2 Watu wangu hutaka shauri kwa kipande cha mti, na fimbo yao huwatolea uaguzi; maana roho ya uzinzi imewapotosha, wakawacha Mungu wao. 13 Ayu 31:9,10;Amo 7:17;Rum 1:28 Hutoa dhabihu juu ya vilele vya milima, na kufukiza uvumba juu ya vilima, chini ya mialoni na milibua na miela, kwa kuwa uvuli wake ni mwema; kwa sababu hiyo binti zenu huzini, na bibi arusi zenu hufanya uasherati. 14 Sitawaadhibu binti zenu wazinipo, wala bibi arusi zenu wafanyapo uasherati; maana wenyewe huenda kando pamoja na wanawake wazinzi, hutoa dhabihu pamoja na makahaba; na watu hawa wasiofahamu wataangamia.
15 Hos 9:15;Amo 4:4;8:14 Ingawa wewe, Israeli, unafanya uzinzi, lakini asiasi Yuda; nanyi msiende Gilgali wala msipande mpaka Beth-aveni, wala msiape mkisema, Aishivyo BWANA. 16 Kwa maana Israeli ametenda kwa ukaidi, kama ndama mkaidi; sasa je! BWANA atawalisha kama mwana-kondoo katika mahali penye malisho mazuri.4:16 Katika Kiebrania ni penye nafasi.17 Mit 15:14 Efraimu amejiungamanisha na sanamu; mwache. 18 Kileo chao kimegeuka kuwa uchungu; huzini daima; wakuu wake hupenda aibu. 19 Upepo umemfunika kwa mbawa zake; nao watatahayarika kwa sababu ya dhabihu zao.