1 Ole wake yeye aliyeasi na kutiwa unajisi, mji wa udhalimu! 2 Yer 22:21;5:3 Hakuitii sauti; hakukubali kurudiwa; hakumwamini BWANA; hakumkaribia Mungu wake. 3 Wakuu wake walio ndani yake ni simba wangurumao; mahakimu wake ni mbwamwitu wa jioni; wasiobakiza kitu chochote mpaka asubuhi. 4 Yer 23:11;Eze 22:26 Manabii wake ni watu hafifu, wadanganyifu; makuhani wake wamepatia unajisi patakatifu, wameifanyia sheria udhalimu. 5 Kum 32:4;Zab 99:3,4 BWANA kati yake ni mwenye haki; hatatenda uovu; kila asubuhi hudhihirisha hukumu yake, wala hakomi; bali mtu asiye haki hajui kuona haya. 6 Nimekatilia mbali mataifa, minara yao ina ukiwa; nimeziharibu njia kuu zao, hata hapana mmoja apitaye; miji yao imeangamizwa; hamna mtu hata mmoja, wala hapana akaaye huko. 7 Mwa 6:12 Nilisema, Hakika utaniogopa, utakubali kurudiwa; ili yasikatiliwe mbali makao yake, sawasawa ya yote niliyoagiza katika habari zake; lakini waliondoka mapema na kuyaharibu matendo yao yote.
8 Mit 20:22;Yoe 3:2 Basi ningojeeni, asema BWANA, hata siku ile nitakapoondoka kuteka mateka; maana nimeazimia kuwakusanya mataifa, ili nizikutanishe falme, nipate kuwamwagia ghadhabu yangu; naam, ukali wote wa hasira yangu; kwa maana dunia yote itateketezwa kwa moto wa wivu wangu.
9 Maana hapo ndipo nitakapowarudishia mataifa lugha iliyo safi, wapate kuliitia jina la BWANA, wamtumikie kwa nia moja. 10 Zab 68:31;Mal 1:11;Mdo 8:27 Maana toka nchi iliyo mbali na mito ya Kushi, waniombao dua, yaani, binti za watu wangu waliotawanyika, wataleta matoleo yangu. 11 Mt 3:9 Siku ile hutaaibishwa kwa matendo yako yote uliyoniasi; maana hapo nitawaondoa watu wako wanaojigamba na kujivuna, wasiwe kati yako, wala hutatakabari tena katika mlima wangu mtakatifu. 12 Isa 14:32;57:15;Mt 5:3;Lk 6:20 Lakini nitabakiza ndani yako watu walioonewa na maskini, nao watalitumainia jina la BWANA. 13 Ufu 14:5 Mabaki ya Israeli hawatatenda uovu, wala kusema uongo; wala ulimi wa hadaa hautakuwa kinywani mwao; kwa maana watakula na kulala, wala hapana mtu atakayewatisha.
14 Zab 14:7 Imba, Ee binti Sayuni; piga kelele, Ee Israeli;
Furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, Ee binti Yerusalemu.
15 Yn 1:49;Eze 48:35;Ufu 21:3 BWANA ameziondoa hukumu zako,
Amemtupa nje adui yako;
Mfalme wa Israeli, naam, yeye BWANA, yuko katikati yako;
Hutaogopa uovu tena.
16 Isa 35:3 Katika siku ile Yerusalemu utaambiwa,
Usiogope, Ee Sayuni; mikono yako isilegee.
17 BWANA, Mungu wako, yuko katikati yako shujaa awezaye kuokoa;
Atakushangilia kwa furaha kuu,
Atakutuliza katika upendo wake,
Atakufurahia kwa kuimba.
18 Omb 2:6 Nitawakusanya wanaousikitikia mkutano wa ibada, hao waliokuwa wa kwako; ambao mzigo uliokuwa juu yake ulikuwa fedheha kwao. 19 Tazama, wakati huo nitawapatiliza watu wote wanaokutesa; nami nitamponya yeye achechemeaye, nami nitamkusanya yeye aliyefukuzwa; nami nitawafanya msifiwe na kujulikana, hao ambao aibu yao ilikuwa katika dunia yote. 20 Zab 22:27 Wakati huo nitawaingizeni, na wakati huo nitawakusanya; kwa maana nitawafanya ninyi msifiwe na mjulikane, miongoni mwa watu wote wa dunia, nitakapowarudisha wafungwa wenu mbele ya macho yenu, asema BWANA.