1 Kila apendaye mafundisho hupenda maarifa;
Bali yeye achukiaye kulaumiwa ni kama mnyama.
2 Mtu mwema atapata upendeleo kwa BWANA;
Bali mtu wa hila atahukumiwa naye.
3 Mtu hatathibitika kwa njia ya uovu;
Shina la mwenye haki halitaondolewa kamwe.
4 Mwanamke mwema ni taji la mumewe;
Bali aaibishaye ni kama kuoza mifupani mwake.
5 Mawazo ya mwenye haki ni adili;
Bali mashauri ya mtu mwovu ni hadaa.
6 Maneno ya waovu huotea damu;
Bali kinywa cha wanyofu kitawaokoa.
7 Waovu huangamia, hata hawako tena;
Bali nyumba ya mwenye haki itasimama.
8 Mtu atasifiwa kwa kadiri ya akili zake;
Bali mwenye moyo wa ukaidi atadharauliwa.
9 Afadhali mtu anayedharauliwa, ikiwa ana mtumwa,
Kuliko ajisifuye, ikiwa anahitaji chakula.
10 Mwenye haki huufikiri uhai wa mnyama wake;
Bali huruma za mtu mwovu ni ukatili.
11 Alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele;
Bali afuataye mambo ya upuzi hana ufahamu.
12 Asiye haki hutamani nyavu za wabaya;
Bali shina lao wenye haki huleta matunda.
13 Katika kosa la midomo kuna mtego kwa mbaya;
Bali mwenye haki atatoka katika taabu.
14 Mtu atashiba mema kwa matunda ya kinywa chake;
Na atarudishiwa matendo ya mikono yake.
15 Njia ya mpumbavu imenyoka machoni pake mwenyewe;
Bali yeye aliye na hekima husikiliza shauri.
16 Ghadhabu ya mpumbavu hujulikana mara;
Bali mtu mwerevu husitiri aibu.
17 Atamkaye maneno ya kweli hufunua haki;
Bali shahidi wa uongo hutamka hila.
18 Kuna anenaye bila kufikiri, kama kuchoma kwa upanga;
Bali ulimi wa mwenye haki ni afya.
19 Mdomo wa kweli utathibitishwa milele;
Bali ulimi wa uongo ni wa kitambo tu.
20 Hila imo mioyoni mwao wafikirio uovu;
Bali wafanyao mashauri ya amani, kwao kuna furaha.
21 Mwenye haki hatapatikana na msiba wowote;
Bali wasio haki watajazwa mabaya.
22 Midomo ya uongo ni chukizo kwa BWANA;
Bali watendao uaminifu ndio furaha yake.
23 Mwanadamu mwenye busara husitiri maarifa;
Bali moyo wa wapumbavu hutangaza upumbavu.
24 Mkono wa mwenye bidii utatawala;
Bali mvivu atalipishwa kodi.
25 Uzito katika moyo wa mtu huuinamisha;
Bali neno jema huufurahisha.
26 Mwenye haki ni kiongozi wa mwenzake;
Bali njia ya wasio haki huwakosesha.
27 Mtu mvivu hapiki mawindo yake;
Bali mwenye bidii anazo mali za thamani.
28 Katika njia ya haki kuna uhai;
Wala hakuna mauti katika mapito yake.