Publicidade

Provérbios 15

1 Jawabu la upole hugeuza hasira;

Bali neno liumizalo huchochea ghadhabu.

2 Ulimi wa mwenye hekima hutamka maarifa vizuri;

Bali vinywa vya wapumbavu humwaga upumbavu.

3 Macho ya BWANA yako kila mahali;

Yakimchunguza mbaya na mwema.

4 Ulimi safi ni mti wa uzima;

Bali ukorofi wa ulimi huvunja moyo.

5 Mpumbavu hudharau kurudiwa na babaye;

Bali yeye aangaliaye maonyo hupata busara.

6 Katika nyumba ya mwenye haki mna akiba nyingi;

Bali mapato ya mtu mbaya huwa taabu tu.

7 Midomo ya mwenye haki hueneza maarifa;

Bali moyo wa mpumbavu haufanyi hivyo.

8 Sadaka ya mtu mbaya ni chukizo kwa BWANA;

Bali maombi ya mtu mnyofu ni furaha yake.

9 Njia ya mtu mbaya ni chukizo kwa BWANA;

Bali humpenda mtu afuatiaye wema.

10 Adhabu kali ina yeye aiachaye njia;

Naye achukiaye kukemewa atakufa.

11 Kuzimu na Uharibifu viko wazi mbele za BWANA;

Si zaidi basi, mioyo ya wanadamu?

12 Mwenye mzaha hapendi kukaripiwa;

Wala yeye hawaendei wenye hekima.

13 Moyo wa furaha huchangamsha uso;

Bali kwa huzuni ya moyo roho hupondeka.

14 Moyo wa mwenye ufahamu hutafuta maarifa;

Bali kinywa cha wapumbavu hula upumbavu.

15 Siku zote za mtu ateswaye ni mbaya;

Bali ukunjufu wa moyo ni karamu ya daima.

16 Kuwa na mali chache pamoja na kumcha BWANA;

Ni bora kuliko mali nyingi pamoja na taabu.

17 Chakula cha mboga palipo na upendo;

Ni bora kuliko ng'ombe aliyenona pamoja na kuchukiana.

18 Mtu wa hasira huchochea ugomvi;

Bali asiye mwepesi wa hasira hutuliza mashindano.

19 Njia ya mtu mvivu ni kama boma la miiba;

Bali mapito yao wenye unyofu hufanyika njia kuu.

20 Mwana mwenye hekima humfurahisha babaye;

Bali mpumbavu humdharau mamaye.

21 Upumbavu ni furaha kwake aliyepungukiwa na akili;

Bali mwenye ufahamu huunyosha mwenendo wake.

22 Pasipo ushauri mipango vuhunjika;

Bali kwa wingi wa washauri huthibitika.

23 Mtu hulifurahia jibu la kinywa chake;

Na neno linenwalo wakati wa kufaa ni jema kama nini!

24 Kwa mtu mwenye akili njia ya uhai huenda juu;

Ili atoke katika kuzimu chini.

25 BWANA ataing'oa nyumba ya mwenye kiburi;

Bali atauthibitisha mpaka wa mjane.

26 Ushauri mbaya ni chukizo kwa BWANA;

Bali maneno yapendezayo ni safi.

27 Atamaniye faida huifadhaisha nyumba yake mwenyewe;

Bali achukiaye zawadi ataishi.

28 Moyo wa mwenye haki hufikiri jinsi atakavyojibu;

Bali kinywa cha wasio haki humwaga mabaya.

29 BWANA yuko mbali na wasio haki;

Bali huisikia sala ya mwenye haki.

30 Mng'ao wa macho huufurahisha moyo;

Habari njema huinenepesha mifupa.

31 Sikio lisikilizalo lawama yenye uhai

Litakaa kati yao wenye hekima.

32 Akataaye maonyo huidharau nafsi yake mwenyewe;

Bali yeye asikilizaye lawama hujipatia ufahamu.

33 Kumcha BWANA ni maonyo ya hekima;

Na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu.

Veja também

Publicidade
Bíblia Online Bíblia Online

Bíblia Online • Versão: 2026-06-22_10-02-25-