KITABU CHA PILI
1 Mwana mwenye hekima humfurahisha babaye;
Bali mwana mpumbavu ni mzigo wa mamaye.
2 Hazina za uovu hazifaidii kitu;
Bali haki huokoa na mauti.
3 BWANA hataiacha nafsi ya mwenye haki ife na njaa;
Bali tamaa ya mtu mwovu huisukumia mbali.
4 Atendaye mambo kwa mkono mlegevu huwa maskini;
Bali mkono wake aliye na bidii hutajirisha.
5 Akusanyaye wakati wa joto ni mwana mwenye hekima;
Bali asinziaye wakati wa mavuno ni mwana mwenye kuaibisha.
6 Baraka humkalia mwenye haki kichwani;
Bali jeuri hufunika kinywa chake mtu mwovu.
7 Kuwakumbuka wenye haki huwa na baraka;
Bali jina la mtu mwovu litaoza.
8 Aliye na akili moyoni mwake atapokea agizo;
Bali mpumbavu mwenye maneno mengi ataanguka.
9 Aendaye kwa unyofu huenda salama;
Bali apotoshaye njia zake atajulikana.
10 Akonyezaye kwa jicho huleta masikitiko;
Bali mpumbavu mwenye maneno mengi ataanguka.
11 Kinywa chake mwenye haki ni chemchemi ya uzima;
Bali jeuri hufunika kinywa chake mtu mwovu,
12 Kuchukiana huleta fitina;
Bali kupendana husitiri makosa yote.
13 Hekima hupatikana midomoni mwa mwenye ufahamu;
Bali fimbo hufaa kwa mgongo wake asiye na ufahamu.
14 Watu wenye akili huweka akiba ya maarifa;
Bali kinywa cha mpumbavu ni uangamivu ulio karibu.
15 Mali ya tajiri ndio ngome yake;
Ufukara wa maskini ndio umwangamizao.
16 Kazi yake mwenye haki huuelekea uzima;
Mazao ya wabaya huielekea dhambi.
17 Akubaliye kurudiwa huwa katika njia ya uzima;
Bali yeye aachaye maonyo hukosa.
18 Yeye afichaye chuki ana midomo ya uongo,
Na yeye asingiziaye ni mpumbavu.
19 Katika wingi wa maneno hapakosi kuwa na maovu;
Bali yeye azuiaye midomo yake hufanya akili.
20 Ulimi wa mwenye haki ni kama fedha safi;
Moyo wa mtu mbaya haufai kitu.
21 Midomo ya mwenye haki hulisha watu wengi;
Bali wapumbavu hufa kwa kuwa hawana ufahamu.
22 Baraka ya BWANA hutajirisha,
Wala hachanganyi huzuni nayo.
23 Kwa mpumbavu kutenda maovu ni kama mchezo;
Bali mtu mwenye ufahamu ana hekima.
24 Aogopacho mtu asiye haki ndicho kitakachomjilia;
Na wenye haki watapewa matakwa yao.
25 Kisulisuli kikiisha pita asiye haki hayuko tena;
Bali mwenye haki ni msingi wa milele.
26 Kama siki menoni, na kama moshi machoni,
Ndivyo alivyo mtu mvivu kwa hao waliomwajiri.
27 Kumcha BWANA kwaongeza siku za mtu;
Bali miaka yao wasio haki itapunguzwa.
28 Matumaini yao wenye haki yatakuwa furaha;
Bali matarajio yao wasio haki yatapotea.
29 Njia ya BWANA ni kimbilio lake mtu mkamilifu;
Bali ni uharibifu kwao watendao maovu.
30 Mwenye haki hataondolewa milele;
Bali wasio haki hawatakaa katika nchi.
31 Kinywa cha mwenye haki hutoa hekima;
Bali ulimi wa ukaidi utakatiliwa mbali.
32 Midomo ya mwenye haki huyajua yatakayokubaliwa;
Bali kinywa chao wasio haki hunena ukaidi.