Publicidade

Provérbios 21

1 Moyo wa mfalme huwa katika mkono wa BWANA;

Kama mifereji ya maji huugeuza popote apendapo.

2 Kila njia ya mtu ni sawa machoni pake mwenyewe;

Bali BWANA huipima mioyo.

3 Kutenda haki na hukumu

Humpendeza BWANA kuliko kutoa sadaka.

4 Mwenye kiburi na moyo wa majivuno,

Taa yake ni dhambi.

5 Mawazo ya wenye bidii huuelekea utajiri tu;

Bali kila mwenye pupa huuelekea uhitaji.

6 Kupata akiba ya mali kwa ulimi wa uongo

Ni moshi upeperushwao; ni kutafuta mauti.

7 Jeuri ya wabaya itawaondolea mbali;

Kwa sababu wamekataa kutenda hukumu.

8 Njia yake aliyelemewa na dhambi imepotoka sana;

Bali mtu aliye safi, kazi yake ni sawasawa.

9 Ni afadhali kukaa katika pembe ya darini,

Kuliko katika nyumba pana pamoja na mwanamke mgomvi.

10 Nafsi ya mtu mbaya hutamani uovu;

Jirani yake hapati fadhili machoni pake.

11 Mwenye mzaha aadhibiwapo, mjinga hupata hekima;

Na mwenye hekima afundishwapo, hupokea maarifa.

12 Mwenye haki huitafakari nyumba ya mtu mbaya;

Jinsi wabaya waangushwavyo wakaangamia.

13 Azibaye masikio yake asisikie kilio cha maskini,

Yeye naye atalia, lakini hatasikiwa.

14 Kipawa cha siri hutuliza hasira;

Na rushwa bindoni humliza ghadhabu kali.

15 Ni furaha yao wenye haki kutenda hukumu;

Lakini ni uharibifu kwao watendao maovu.

16 Mtu aikosaye njia ya busara

Atakaa katika mkutano wao waliokufa.

17 Mtu apendaye anasa atakuwa maskini;

Apendaye mvinyo na mafuta hatakuwa tajiri.

18 Mtu asiye haki ni fidia ya wenye haki;

Naye afanyaye hila ni badala ya watu wa adili.

19 Ni afadhali kukaa katika nchi ya nyika;

Kuliko na mwanamke mgomvi, mchokozi.

20 Kuna hazina ya thamani na mafuta katika maskani ya mwenye hekima;

Bali mwanadamu aliye mpumbavu huyameza.

21 Aandamaye haki na fadhili,

Ataona uhai na haki na heshima.

22 Mwenye hekima huupandia mji wao wenye nguvu;

Na kuziangusha nguvu za tumaini lao.

23 Mtu azuiaye kinywa chake na ulimi wake,

Atajilinda nafsi yake na taabu.

24 Mwenye kiburi na kutakabari, jina lake ni mbishi;

Hutenda mambo katika majivuno ya kiburi chake.

25 Matakwa yake mtu mvivu humwua,

Kwa maana mikono yake hukataa kufanya kazi.

26 Kuna atamaniye kwa choyo mchana kutwa;

Bali mwenye haki hutoa wala hanyimi.

27 Sadaka ya wasio haki ni chukizo;

Si zaidi sana ailetapo mwenye nia mbaya!

28 Shahidi wa uongo atapotea;

Bali mtu asikiaye atasema maneno yadumuyo.

29 Asiye haki huufanya uso wake kuwa mgumu;

Bali mtu mnyofu huzifikiri njia zake.

30 Hapana hekima, wala ufahamu,

Wala shauri, juu ya BWANA.

31 Farasi huwekwa tayari kwa siku ya vita;

Lakini BWANA ndiye aletaye wokovu.

Veja também

Publicidade
Bíblia Online Bíblia Online

Bíblia Online • Versão: 2026-06-15_21-32-39-